NEMC YATAKA CHANGAMOTO ZA MAZINGIRA KUBADILISHWA KUWA MIRADI
DAR ES SALAAM: Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limetaka kujengwa kwa mifumo itakayowezesha ubunifu na fursa za mazingira kubadilishwa kuwa miradi inayotekelezeka, kufadhiliwa na kukua.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkurugenzi wa Tafiti za Mazingira wa NEMC, Dkt. Careen Kahangwa, kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa baraza hilo, Dkt. Immaculate Sware Semesi, wakati wa hafla ya kufunga Tanzania Green Summit 2026, iliyofanyika jana, Septemba 16, 2026, katika Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Dkt. Kahangwa amesema mfumo huo unapaswa kuwaunganisha wabunifu, wajasiriamali na jamii na ujuzi, teknolojia, masoko, taasisi za fedha pamoja na washirika wa maendeleo.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuhakikisha mawazo ya ubunifu hayabaki kwenye mashindano, maonesho au miradi ya majaribio pekee, bali yanabadilika kuwa biashara endelevu, ajira, uwekezaji na suluhisho la changamoto za mazingira na mabadiliko ya tabianchi.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kujenga ushirikiano wa kudumu utakaowezesha maazimio ya kongamano hilo kutafsiriwa kuwa hatua na matokeo yanayopimika.
“Tanzania Green Summit haipaswi kuwa tukio la siku mbili pekee, bali iwe sehemu ya mchakato endelevu wa kuunganisha sera, ubunifu, fedha, teknolojia na utekelezaji,” amesema.
Ameongeza kuwa fursa zilizojadiliwa na ushirikiano ulioanzishwa wakati wa mkutano huo vinapaswa kufuatiliwa ili kupima matokeo ya hatua zitakazochukuliwa.
Tanzania Green Summit 2026 imefanyika Septemba 15 na 16, 2026, ikiwa na kaulimbiu “Turning Climate Action into Opportunity”, inayomaanisha “Kugeuza Hatua za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kuwa Fursa.”








