NSSF YAJIPANGA KUFIKIA WANACHAMA MILIONI 6.6 KUFIKAPO 2031
Dar es salaam - Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeweka mkakati wa kupanua wigo wa hifadhi ya jamii nchini kwa kuongeza idadi ya wanachama wachangiaji kutoka 2,144,906 waliokuwepo Juni 2026 hadi 6,609,403 ifikapo mwaka 2030/31, hatua inayolenga kuwafikia Watanzania wengi zaidi katika sekta rasmi na isiyo rasmi.
Akizingumza wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu na mafanikio ya Mfuko katika mkutano na wahariri wa vyombo vya habari ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba amesema ongezeko hilo ni sawa na asilimia 209 na litaenda sambamba na jitihada za kuimarisha huduma za hifadhi ya jamii.
Mshomba amesema NSSF imepata msingi wa kufikia lengo hilo kutokana na ukuaji wa wanachama katika kipindi cha mwaka wa fedha 2020/21 hadi 2025/26, ambapo idadi iliongezeka kwa asilimia 130 kutoka 932,112 hadi 2,144,906, huku wanachama wapya 1,486,930 wakisajiliwa katika kipindi hicho.
Amesema mkakati huo pia unalenga kuimarisha uwezo wa Mfuko kifedha, ambapo thamani ya NSSF inatarajiwa kuongezeka kutoka Sh11.42 trilioni Juni 2026 hadi Sh24.75 trilioni Juni 2031, huku thamani ya uwekezaji ikipanda kutoka Sh9.61 trilioni hadi Sh20.35 trilioni. Aidha, Mfuko unalenga kukusanya michango yenye thamani ya Sh21.12 trilioni na kupata mapato ya uwekezaji ya Sh5.28 trilioni katika kipindi cha Julai 2026 hadi Juni 2031.
Katika kupanua huduma kwa wananchi walio nje ya ajira rasmi, Mshomba amesema NSSF imeendelea kutekeleza Skimu ya Hifadhi ya Jamii kwa wananchi waliojiajiri iliyozinduliwa Februari 2026, inayolenga makundi kama wakulima, wavuvi, waendesha bodaboda na bajaji, mamalishe na babalishe, wachimbaji wadogo, machinga na wengine. Amesema hadi Juni 30, 2026, skimu hiyo ilikuwa na wanachama 592,791 na inalenga kuongeza wanachama wapya 279,371 katika mwaka wa fedha 2026/27.
Amesema ongezeko hilo la wanachama linaenda sambamba na kuboresha mafao na huduma, ambapo malipo ya mafao yataongezeka kutoka Sh594.33 bilioni mwaka 2020/21 hadi Sh1.16 trilioni mwaka 2025/26, huku kiwango cha mkupuo kikiongezwa.




