UCHUMI WA BLUU: TANZANIA YAWEKA SHERIA IMARA KULINDA UTAJIRI WA BAHARI
DAR ES SALAAM: Wizara ya Katiba na Sheria imesema kuna umuhimu wa kuendelea kuoanisha sheria za Tanzania zinazosimamia uchumi wa bluu na sheria za kimataifa ili kuimarisha ulinzi na matumizi endelevu ya rasilimali za bahari.
Akizungumza katika Kongamano la Kimataifa la Tano la Uchumi wa Bluu lililofanyika kwa siku tatu kuanzia Septemba 7 hadi 9, 2026, Mkurugenzi Msaidizi wa Sehemu ya Utatuzi wa Migogoro kwa Njia Mbadala kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Felix Bullet Shakila, amesema kongamano hilo limewezesha wadau kutoa mawazo kuhusu namna bora ya kuimarisha sekta hiyo kupitia sheria madhubuti.
Shakila amesema moja ya mambo yaliyoibuka katika kongamano hilo ni umuhimu wa kuhakikisha sheria za ndani zinaendana na sheria na mikataba ya kimataifa ili kuepusha migongano ya kisheria, hususan katika masuala yanayohusu mahusiano baina ya nchi na matumizi ya rasilimali za bahari.
Amesema Tanzania tayari imechukua hatua katika kusimamia rasilimali zake za bahari kupitia sheria mbalimbali, ikiwemo sheria zinazohusu ulinzi wa maliasili na utajiri wa nchi pamoja na usimamizi wa mipaka na mamlaka za nchi.
Kwa upande wake, kamishna wa katiba na sheria- jumuiya ya wanafunzi taasisi za elimu ya juu Tanzania, ARON MZELELA SENI akiongea mara baada ya kutembelea banda la Katiba na Sheria amesema masuala ya bahari yanaongozwa kwa kiasi kikubwa na sheria za kimataifa, ikiwemo Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Sheria za Bahari (UNCLOS), unaoweka misingi ya matumizi na usimamizi wa rasilimali za bahari.
Saini amesema Tanzania inapaswa kuongeza juhudi za kufanya domestication ya sheria na mikataba ya kimataifa ambayo imejiunga nayo kwa kutunga sheria za ndani zitakazowezesha utekelezaji wake kwa ufanisi zaidi.
Amesema hatua hiyo itasaidia kuimarisha usimamizi wa rasilimali za bahari na kuhakikisha uchumi wa bluu unakuwa endelevu, huku wananchi wakinufaika kupitia shughuli mbalimbali kama usafirishaji wa majini, uvuvi, chakula na utalii wa baharini.




