SHEIKH JALALA AWATAKA WAISLAMU KUENDELEZA VIKAO VYA MAULIDI
MWANZA, Septemba 4, 2026 — Sheikh Mkuu wa Jumuiya ya Shia Tanzania (TIC), Maulana Sheikh Hemed Jalala Mwakindenge, amewataka Waislamu kuendelea na vikao vya Maulidi kwa ajili ya kumkumbuka na kumswalia Mtume Muhammad (s.a.w.w.) pamoja na kujifunza maadili yake.
Sheikh Jalala ametoa kauli hiyo jijini Mwanza wakati akizungumza katika hafla ya Maulidi iliyoandaliwa na Sheikh wa Mkoa wa Mwanza wa TIC, Sheikh Hashim.
Amesema vikao vya Maulidi vina umuhimu mkubwa katika kuwakumbusha Waislamu mafundisho na mwenendo wa Mtume Muhammad (s.a.w.w.), huku akisisitiza umuhimu wa kujifunza na kuzingatia maadili yake katika maisha ya kila siku.
Aidha, Sheikh Jalala amewataka Waislamu kudumisha vikao vya dua na dhikri, akieleza kuwa ni miongoni mwa njia za kuimarisha imani, kuomba msamaha na kuleta baraka katika jamii.
Amewahimiza waumini kuendeleza utamaduni huo kwa kuzingatia mafundisho sahihi ya dini.
Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi wa dini mbalimbali, wakiongozwa na mwenyeji wao, Sheikh wa Mkoa wa Mwanza wa Bakwata, Sheikh Hassan Kabeke.








