Breaking News

TANZANIA KUFIKISHA HUDUMA ZA KIDIJITALI VIJIJINI

DAR ES SALAAM - Tanzania imepiga hatua kubwa katika ujenzi wa miundombinu ya kidijitali na upatikanaji wa huduma za umma kwa njia ya kielektroniki kupitia Mradi wa Digital Tanzania (DTP), huku utekelezaji wake ukitarajiwa kukamilika rasmi Oktoba 31, 2026.

Mkurugenzi wa TEHAMA kutoka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Priscus Kiwango, amesema hayo Septemba 14, 2026, wakati akizungumza na waandishi wa habari kando ya mkutano wa wadau wa mradi huo.

Kiwango amesema mradi huo ulioanza mwaka 2021 kwa ufadhili wa mkopo wa Dola za Marekani milioni 150 kutoka Benki ya Dunia, umewezesha kuboresha miundombinu ya mawasiliano, kuongeza upatikanaji wa intaneti na kuimarisha utoaji wa huduma za Serikali kwa kutumia teknolojia.

Amesema mradi umewezesha kujengwa na kuboreshwa kwa minara ya mawasiliano, hususan katika maeneo ya vijijini yaliyokuwa yakikabiliwa na changamoto ya huduma za mawasiliano, ambapo wananchi sasa wanaweza kupata huduma kupitia mitandao ya 3G na 4G
Aidha, amesema taasisi za Serikali hadi ngazi ya Serikali za Mitaa zimeunganishwa katika mifumo mbalimbali ya kidijitali, ikiwemo PEPMIS unaotumika kupima utendaji wa watumishi wa umma pamoja na Mfumo wa Daktari wa Huduma za Serikali unaowezesha wananchi kupata taarifa kuhusu huduma, muda wa kuzipata na gharama zake.

Kwa upande wake, Mratibu wa Mradi wa Digital Tanzania, Bakari Mwamguguyo, amesema utekelezaji wa mradi huo umejikita katika maeneo matatu makuu ambayo ni Ekolojia ya Kidijitali inayohusisha sheria, miongozo na sera za TEHAMA, uunganishaji wa kidijitali na kuwajengea uwezo watumishi.

Amesema minara mipya 758 imejengwa huku minara 304 ikiboreshwa kutoka teknolojia ya 2G kwenda 3G na 4G, huku uwezo wa intaneti ukiongezwa hadi Gbps 60, ambapo Gbps 40 ni kwa Tanzania Bara na Gbps 20 kwa Zanzibar.

Mwamguguyo amesema mradi pia umewezesha kuanzishwa kwa vituo 32 vya huduma pamoja (One-Stop Service Centers) katika majengo ya Posta, vinavyowawezesha wananchi kupata huduma za NIDA, RITA, Jeshi la Polisi na Land Registry katika eneo moja.
Ameongeza kuwa watumishi wa umma wapatao 500 wamepatiwa mafunzo kuhusu teknolojia za kisasa, ikiwemo matumizi ya akili mnemba (AI), huku watumishi 50 wakipelekwa kusoma nje ya nchi katika ngazi ya uzamili.

Naye Mkurugenzi wa Mawasiliano na Miundombinu wa Wizara ya Mawasiliano, Teknolojia ya Habari na Ubunifu Zanzibar, Issa Bakari, amesema mradi huo umewezesha kuanzishwa kwa Zanzibar Digital Services Directory (ZGSD), ZanPortal pamoja na vituo viwili vya One-Stop Center vilivyojengwa Posta Kijangwani Unguja na Chakechake Pemba.

Bakari amesema zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa Zanzibar sasa wanafikiwa na huduma za mawasiliano kuanzia 2G hadi 5G kupitia minara 63 iliyojengwa katika utekelezaji wa mradi huo.

Amesema kutokana na mafanikio yaliyopatikana, Serikali imeanza mazungumzo na Wizara ya Fedha pamoja na Benki ya Dunia kuhusu uwezekano wa kuingia katika awamu ya pili ya Mradi wa Digital Tanzania, itakayolenga kukamilisha na kuendeleza maeneo ambayo hayajakamilishwa katika awamu ya kwanza.