TANZANIA YAHIMIZA UTEKELEZAJI WA MAAZIMIO YA UCHUMI WA BULUU
DAR ES SALAAM: Tanzania imewataka wadau wa uchumi wa buluu kuhakikisha maazimio, tafiti na mawazo yaliyotokana na Mkutano wa Tano wa Kimataifa wa Uchumi wa Buluu yanatafsiriwa kuwa vitendo, miradi na ushirikiano wenye matokeo yanayopimika.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI), Peter Olekashe, amesema maendeleo ya uchumi wa buluu yanahitaji mtazamo jumuishi unaozingatia uwekezaji, teknolojia, usalama wa baharini, uhifadhi wa mazingira na matumizi bora ya rasilimali za majini.
Amesema majadiliano ya mkutano huo yameainisha fursa mbalimbali zinazoweza kuchangia ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii, ikiwemo uvuvi, usafiri wa baharini, bandari, utalii, viwanda vya baharini na biashara ya kikanda.
Olekashe amesema matumizi ya akili bandia (AI), mifumo ya kidijitali na teknolojia mpya yana nafasi muhimu katika kuongeza ufanisi wa bandari na sekta nyingine za uchumi wa buluu, akisisitiza kuwa ushindani wa siku zijazo unategemea maandalizi yanayofanyika sasa.
Kwa Tanzania, amesema rasilimali za bahari na maeneo ya pwani zina uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira, kuongeza mapato ya taifa na kuvutia uwekezaji, hivyo kuna umuhimu wa kuimarisha sheria, sera, rasilimaliwatu na ushirikiano wa kitaasisi.
Aidha, amewapongeza Mkurugenzi wa chuo cha DMI, Profesa Gurumo, pamoja na uongozi na wafanyakazi wa chuo hicho kwa maandalizi ya mkutano huo, sambamba na wadau wa ndani na kimataifa kwa mchango wao katika kujadili maendeleo ya uchumi wa buluu.
Amewataka washiriki kuendeleza mtandao na ushirikiano ulioanzishwa kupitia mkutano huo, pamoja na kuendelea kuwekeza katika utafiti, ubunifu na teknolojia kwa ajili ya kujenga uchumi wa buluu wenye tija, usalama, ushindani na endelevu.
Aidha, amewaalika wageni wa kimataifa kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii nchini, hususan Dar es Salaam na Zanzibar, akisisitiza kuwa Tanzania ni nchi ya amani, ukarimu na utulivu.




