WADAU WA SIASA TANZANIA WASISITIZA MARIDHIANO KABLA YA KATIBA
Watanzania wameshauriwa kuponya majeraha ya Oktoba 29, 2025 kwa kuzungumza kwanza kabla ya kuanzisha mchakato wa katiba mpya ili kuepuka migawanyiko.
Kauli hiyo iliyotolewa na mmoja wa wadau wa siasa nchini John Mrema ni moja nya michango kadhaa ya wadau wa siasa nchini kuhusu mwenendo wa kisiasa na hatima yab taifa hili kuelekea maridhiano.
Pamoja na kauli hiyo ya Mrema, Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa, Juma Khatib Ali, naye alisema kuwa wakati wa kunyoosheana vidole umekwisha na taifa linapaswa kujengwa badala ya kubomoa.
Kauli hizo zimetolewa wakati mikutano ya pamoja kati ya wanasiasa na asasi za kiraia ikishika kasi ikiwa ni juhudi za kutafuta maridhiano na amani kufuatia vurugu zilizotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Mikutamo hiyo imekuwa chachu ya tafakuri tunduizi kwa wanasiasa na wasomi kujadili mustakabali wa taifa, huku Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, akihimiza wadau kujikita katika hoja zenye suluhu badala ya mabishano, sambamba na mwanasiasa mkongwe James Mbatia aliyesisitiza uwepo wa utashi wa kisiasa na matumizi mazuri ya lugha kufikia maridhiano hayo.
Wakati huo huoWaziri Mkuu na Makamu wa Rais mstaafu, Jaji Joseph Warioba, ameonya dhidi ya dalili za kibaguzi za kidini na kikanda, akisisitiza kurejea kwenye misingi ya amani na usawa iliyoasisiwa tangu zamani.
Pia katika mikutano hiyo, wadau walipinga vikali wazo la kuwaita wapatanishi kutoka nje ya nchi, wakisisitiza kuwa Watanzania wana uwezo wa kukaa wenyewe na kutatua changamoto zao ili kujenga utamaduni wa kujitegemea, msimamo ulioungwa mkono na Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, Ismail Jussa.
Pia Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu, na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Agrey Mwanri, nao wameeleza utayari wa vyama vyao kushirikiana katika kujenga misingi thabiti ya amani na utulivu wa kudumu nchini




