Breaking News

DAR ES SALAAM, JOBURG ZAWA VITUO VIPYA VYA UHARIRI VYA SPUTNIK

Na Mwandishi Wetu - SHIRIKA la habari la kimataifa la Sputnik kutoka nchini Urusi, limefungua rasmi vituo viwili vya uhariri barani Afrika vilivyopo jijini Dar es Salaam, Tanzania na Johannesburg, Afrika Kusini.

Hatua hiyo inalenga kuimarisha uwasilishaji wa habari za ukweli, kuongeza wigo wa habari za bara la Afrika kimataifa, pamoja na kuimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Urusi na nchi za Afrika kuelekea Mkutano wa Tatu wa Urusi na Afrika utakaofanyika Oktoba 28–29 mjini Moscow.

Akizungumza kwa njia ya video wakati wa hafla ya ufunguzi wa kituo cha Dar es Salaam, Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergey Lavrov, alisema vituo hivyo vitawapa watazamaji na wasomaji wa Afrika fursa kubwa zaidi ya kupata taarifa zilizothibitishwa bila kupotoshwa au kuchujwa kwa misingi ya itikadi.

“Leo, wakati nchi za Magharibi zikiendelea kukandamiza sauti zinazotoa mitazamo tofauti duniani kwa kutumia udhibiti wa habari na viwango viwili, umuhimu wa kazi hii hauwezi kupuuzwa,” alisema Lavrov huku akiyashukuru serikali za Tanzania na Afrika Kusini kwa kutoa usaidizi uliowezesha ufunguzi huo.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania, Said Shaib Moussa, alieleza matarajio ya serikali kuwa Sputnik itatoa habari za kanda na dunia kwa uwazi na bila ubaguzi katika nyanja za siasa za kijiografia na maendeleo.

Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Habari kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Kelvin Kanje, aliongeza kuwa ufunguzi huo utawezesha sauti ya Tanzania kusikika zaidi katika jukwaa la kimataifa na kuongeza fursa za ushirikiano wa kitaalamu.

Kwa upande wa Afrika Kusini, Makamu wa Rais wa nchi hiyo, Paul Mashatile, alipongeza hatua hiyo akisema inachangia kuwepo kwa sauti na mitazamo mbalimbali inayochochea mijadala ya kidemokrasia na kuimarisha ushirikiano wa miaka mingi kati ya Urusi na nchi za Afrika
Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Andrey Avetisyan, na Balozi wa Urusi nchini Afrika Kusini, Roman Ambarov, kwa pamoja walisisitiza kuwa uwepo wa Sputnik utakuwa daraja la kufikisha taarifa za ukweli na usawa kati ya pande hizo mbili, hasa katika kipindi ambacho habari zinakabiliwa na changamoto ya upotoshaji.

Mkurugenzi Mkuu wa kundi la vyombo vya habari la Rossiya Segodnya (ambalo Sputnik ni sehemu yake), Dmitry Kiselev, pamoja na Mhariri Mkuu Margarita Simonyan, walieleza kuwa fursa ya kufanya kazi moja kwa moja ndani ya Afrika ni ishara ya uaminifu wa kisekta na itachangia ustawi wa pamoja.

Vituo hivyo vipya vitazalisha maudhui ya habari na vipindi vya podikasti kwa lugha za Kiswahili na Kiingereza, vikirushwa kupitia vituo mbalimbali vya redio barani Afrika vyenye uwezo wa kufikia wasikilizaji zaidi ya milioni 100.
Sputnik Africa ilizinduliwa mwaka 2022 na inatangaza kwa lugha tano ikiwemo Kiswahili, Kiamhari na Oromo, huku ikifanya kazi katika lugha zaidi ya 30 na kuendesha vituo 26 duniani kote.