Breaking News

WAZIRI MKENDA AITAKA BODI MPYA NECTA KULINDA UADILIFU WA MITIHANI

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, amesisitiza umuhimu wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA) kuendelea kulinda uadilifu wa mitihani nchini ili kuhakikisha mfumo wa upimaji unazalisha wataalamu wenye uwezo na weledi katika fani mbalimbali.

Prof. Mkenda ameyasema hayo Oktoba 21, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Bodi Mpya ya Baraza la Mitihani la Tanzania, ambapo amewataka wajumbe wa Bodi hiyo kuendelea kushirikiana na Menejimenti ya Baraza katika kuboresha usimamizi wa mitihani na kuhakikisha viwango vya uadilifu vinaendelea kulindwa.

Aidha, Prof. Mkenda amempongeza Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Prof. Alfred Said Sife, kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema uteuzi huo umeongeza imani kwa uongozi wa Baraza, huku akiwashukuru wajumbe wengine kwa kukubali dhamana hiyo na kuwataka kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na weledi.
Amesema Baraza la Mitihani limeendelea kuwa na utulivu na kufanya kazi vizuri, hivyo ameitaka Menejimenti kuendelea kushirikiana na Bodi katika kuboresha mifumo ya upimaji, ikiwemo kuzingatia uwezo wa mwanafunzi katika kufikiri kwa kina (critical thinking), uchambuzi na kukabiliana na maswali yenye vipengele visivyotabirika, ili kupata wataalamu wenye uwezo wa kutatua changamoto mbalimbali.

Waziri Mkenda amesisitiza kuwa usimamizi madhubuti wa mitihani ni msingi muhimu wa kupata wataalamu bora katika Taifa, akieleza kuwa uadilifu wa mitihani unapaswa kulindwa kwa nguvu zote kwa kuwa matokeo yake yana mchango mkubwa katika kujenga rasilimali watu wenye weledi na uwezo wa kuliongoza Taifa katika sekta mbalimbali.