GF TRUCKS YAKABIDHI GARI, YAFICHUA MAUZO MAKUBWA MAONESHO YA MADINI GEITA
GEITA — Kampuni ya GF Trucks & Equipment imeeleza kuwa Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanayofanyika mkoani Geita yamekuwa na tija, baada ya kupata wateja wapya na kukamilisha mauzo ya magari kwa wachimbaji na kampuni zinazotoa huduma katika sekta ya madini.
Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja Biashara na Masoko wa GF Trucks & Equipment, Smart Deus, amesema kampuni hiyo imefanikiwa kumkabidhi mteja mmoja gari na inatarajia kumkabidhi mteja mwingine zaidi ya magari 10 wakati wa kufungwa kwa maonesho hayo.
Deus amesema GF ilifika katika maonesho hayo ikiwa na magari na vifaa mbalimbali kwa lengo la kuwafikia wachimbaji moja kwa moja, huku mwitikio wa wateja ukiwa mkubwa na baadhi yao kufanya manunuzi.
Amesema maonesho hayo pia yamekuwa sehemu muhimu kwa GF kuimarisha uhusiano wake na wateja katika Kanda ya Ziwa, ikiwa ni mwaka wa 10 kwa kampuni hiyo kushiriki katika shughuli za kibiashara katika eneo hilo.
“Tumeona maonesho yana tija kwa sababu wachimbaji wamekuwa na utayari wa kuja kuulizia bidhaa, wengine wameonyesha interest na wamefanya manunuzi,” amesema Deus.
Aidha, Deus amesema ongezeko la mahitaji ya magari na vifaa vya migodini limeisukuma GF kuwekeza katika GF Vehicle Assemblers, kiwanda kilichopo Kibaha, Mkoa wa Pwani, kinacholenga kuunganisha magari hapa nchini ili kukidhi mahitaji ya soko na kuendana na utekelezaji wa sera ya local content katika sekta ya madini.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Amotech Mine Services, Joffrey Mwasalela, amesema amepata fursa ya kununua na kukabidhiwa gari aina ya Mahindra kupitia maonesho hayo, akisema bidhaa za GF zimekuwa zikisaidia kampuni yake katika shughuli za migodini.
Mwasalela amesema Amotech Mine Services hutoa huduma mbalimbali ikiwemo uchorongaji (drilling), usafirishaji wa malighafi (transportation) na uchimbaji (excavation), ambazo zinahitaji matumizi ya magari na vifaa vinavyopatikana kupitia GF.
Amepongeza uwekezaji unaofanywa na GF katika kuleta magari na vifaa vingi kwenye maonesho hayo, akisema hatua hiyo inawarahisishia wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa kupata vifaa bila kulazimika kusafiri hadi Kibaha, Pwani.
«“Niwapongeze sana GF kwa sababu tunaona uwekezaji mkubwa kabisa. Kuna magari mengi hapa, na wachimbaji wadogo wengi ambao wanashindwa kufika Kibaha wanaweza kupata bidhaa hizi hapa hapa,” amesema Mwasalela.»
GF Trucks & Equipment pia imewashukuru waandaaji wa Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa kwa maandalizi na kuwakaribisha wachimbaji na wadau wa sekta ya madini kutembelea banda lake kwa ajili ya kupata taarifa na huduma mbalimbali.
Kampuni hiyo pia imesema imeungana na taasisi mbalimbali za kifedha ili kuwasaidia wateja kupata fursa za kifedha zinazoweza kurahisisha ununuzi wa magari na vifaa kwa ajili ya shughuli za madini
.





