MAGEREZA WAKANUSHA TAARIFA ZA TUNDU LISSU KUGOMA KULA
Dodoma - JESHI la Magereza Tanzania limekanusha taarifa zinazosambaa katika mitandao ya kijamii zinazodai kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, amegoma kula chakula tangu Oktoba 26, 2026, pamoja na madai kuwa mawakili wake watatu wamezuiwa kuingia gerezani kumwakilisha.
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa Oktoba 27, 2026, na Msemaji wa Jeshi la Magereza, SACP Elizabeth G. Mbezi, jeshi hilo limeeleza kuwa taarifa hizo si za kweli na zinapaswa kupuuzwa ili kuepusha upotoshaji na taharuki katika jamii.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Tundu Lissu yupo salama na hajaanza mgomo wa kula chakula kama inavyodaiwa katika taarifa zinazosambazwa.
Kuhusu madai ya kuzuiwa kwa mawakili wake, Jeshi la Magereza limesema mawakili wanaomuwakilisha wameendelea kuruhusiwa kukutana na mteja wao kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa, baada ya kuthibitishwa kuwa ni mawakili wake halali.
Aidha, jeshi hilo limefafanua kuwa linaendelea kutekeleza majukumu yake ya kuwapokea, kuwahifadhi na kuwarekebisha wafungwa na mahabusu kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu zilizopo.
Limesisitiza kuwa usalama wa watu wote walio chini ya ulinzi wake ni kipaumbele, huku likieleza kuwa linazingatia masuala yote yanayohusu usalama wa wafungwa na mahabusu katika kipindi chote wanachokuwa chini ya ulinzi wa jeshi hilo.
Jeshi la Magereza limewataka wananchi kupuuza taarifa hizo na kuacha kusambaza habari zisizo na ukweli, likisisitiza kuwa kusambaza taarifa za uongo kunaweza kusababisha taharuki katika jamii.





