KAYA 625,000 KUFIKIWA NA BIMA YA AFYA KWA WOTE AWAMU YA PILI - MHE. MCHENGERWA
Mtwara - Serikali kupitia Wizara ya Afya imetangaza mpango wa kusajili kaya 625,000 za wananchi wasio na uwezo katika Awamu ya Pili ya Utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote, sambamba na kupanua wigo wa usajili wananchi wasio uwezo wa kuchangia gharama za bima ili kuhakikisha huduma za afya zinawafikia Watanzania wengi zaidi.
Hayo yamesemwa Oktoba 22, 2026, katika hafla ya kuanza kwa usajili wa bima ya afya kwa wote awamu ya pili wa awamu ya pili mkoani Mtwara, Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema Serikali imejipanga kuhakikisha kila mwananchi anapata fursa ya kujiunga na mfumo wa bima ya afya kulingana na uwezo wake wa kuchangia.
Amesema Awamu ya Pili inalenga kuwafikia wananchi wa makundi mbalimbali wakiwemo wakulima, wafugaji, wavuvi, wafanyabiashara, madereva wa bodaboda, mama lishe na wafanyakazi wa kampuni binafsi ambao wataweza kujiunga na bima kupitia Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) au kampuni binafsi zilizoidhinishwa na Serikali.
Aidha, Mhe. Mchengerwa amesema Serikali itaendelea kugharamia bima kwa wananchi wasio na uwezo, ambao watatambuliwa kupitia mamlaka zinazohusika kwa kushirikisha jamii na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Akizungumzia utekelezaji wa Awamu ya Kwanza, amesema jumla ya kaya 198,709 kati ya kaya 276,004 za wananchi wasio na uwezo zilihakikiwa na kupewa kadi za bima, sawa na asilimia 72 ya lengo, huku Mkoa wa Mtwara ukiongoza kitaifa katika kuwafikia walengwa wa mpango huo.
Mhe. Mchengerwa amewahimiza wananchi kujitokeza kujiandikisha na kuchukua kadi zao za bima ya afya, akisisitiza kuwa ushiriki wa kila mwananchi ni muhimu katika kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuhakikisha huduma bora za afya zinapatikana kwa wote bila kikwazo cha gharama za matibabu.




