Breaking News

MAKAMPUNI YA KICHINA YAAHIDI KUUNGA MKONO MAENDELEO YA TANZANIA

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam - Makampuni ya Kichina yanayofanya kazi nchini Tanzania yameahidi kuendelea kuunga mkono juhudi kubwa za kuleta maendeleo nchini, kwa kushirikiana bega kwa bega na wadau kutoka sekta zote katika kutekeleza DIRA 2050.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CRJE (E.A) LTD na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Makampuni ya Kichina Nchini Tanzania (CEAT), Bw. Jiang Yuntao, wakati akizungumza katika Jukwaa la Maendeleo ya Kimataifa la Makampuni – Tanzania (Phoenix Global Development Forum for Enterprises–Tanzania), lililofanyika Oktoba 3, 2026 katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam.

Jukwaa hilo liliandaliwa kwa pamoja na Phoenix TV na CEAT kwa kaulimbiu ya "Kugundua Afrika Mpya, Kuchunguza Fursa Mpya," na kuhudhuriwa na wageni takriban 100 kutoka serikalini, sekta binafsi na vyuo vikuu.
Miongoni mwa wageni wa heshima waliohudhuria na kutoa hotuba za ufunguzi walikuwa Mhe. Prof. Kitila Mkumbo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji; Bw. Shigeki Komatsubara, Mwakilishi Mkazi wa UNDP nchini Tanzania; na Mhe. Chen Mingjian, Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania.

Bw. Jiang alieleza kuwa historia ya CRJE nchini Tanzania inaanzia kwenye Reli ya Tanzania-Zambia (TAZARA), ambapo tangu mwaka 1969 kampuni mama ya CRJE, China Railway Construction Engineering Group (CRCEG), ilituma wafanyakazi 1,114 kushiriki ujenzi wa reli hiyo.

Alisema Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 iliyozinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan Julai 2025 inalenga kujenga Tanzania iliyo na ustawi, haki, ushirikishwaji na kujitegemea ifikapo 2050, ikiungwa mkono na mradi wa uhuishaji wa TAZARA uliotiwa saini Septemba 2025 na tamko la pamoja la China, Tanzania na Zambia Novemba 2025 la kujenga Ukanda wa Ustawi wa TAZARA.
Kuhusu utekelezaji wa DIRA 2050, alisema CRJE itaendelea kuimarisha misingi ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia miundombinu ya nyumba, barabara, viwanja vya ndege, umeme, maji, umwagiliaji, bandari na uwekezaji.

Alitaja miradi ya hoteli za nyota tano ikiwemo Kilimanjaro Hotel Dar es Salaam, Gran Melia Arusha na Park Hyatt Zanzibar, Daraja la Nyerere, Bandari ya Mtwara, mradi wa umwagiliaji Iringa, laini za umeme Geita, jengo la VIP Terminal 1 lililokamilika ndani ya siku 75, Hoteli ya Johari Rotana, majengo ya Victoria Nobel na Peninsula Noble, na Uwanja wa Arusha wa AFCON mwakani.

Aliongeza kuwa Watanzania wanachukua zaidi ya asilimia 90 ya wafanyakazi katika miradi ya CRJE kupitia mafunzo ya uanagenzi na Programu ya Kukuza Vipaji ya Ufundi wa Kichina kwa Vijana wa Tanzania, pamoja na kuzingatia ujenzi wa kijani na teknolojia za kidijitali.