DIB YATOA ELIMU YA USALAMA WA AMANA KWA WANANCHI
GEITA — Bodi ya Bima ya Amana (DIB) imewataka wananchi kuacha tabia ya kutunza fedha majumbani na badala yake kutumia huduma za benki na taasisi za fedha zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ikieleza kuwa fedha zilizowekwa katika taasisi hizo zinalindwa kupitia mfumo wa bima ya amana.
Akizungumza katika mahojiano maalum na mtandao huu wakati wa Maonesho ya Tisa ya Teknolojia ya Madini Kitaifa yanayoendelea mkoani Geita, Afisa Mwandamizi wa DIB amesema kutunza fedha nyumbani kunaweza kusababisha hasara kwa mtu binafsi na pia kupunguza mzunguko wa fedha katika uchumi.
Amesema fedha zinazohifadhiwa majumbani haziwezi kutumika katika shughuli za uzalishaji kupitia mikopo, tofauti na fedha zinazowekwa benki ambazo zinaweza kukopeshwa kwa wananchi na wafanyabiashara kwa ajili ya kuendesha miradi mbalimbali ya maendeleo.
Kwa upande wa usalama, amesema fedha zilizohifadhiwa nyumbani zinaweza kuibiwa, kuharibiwa na moto au maji, huku wamiliki wake pia wakiwa katika hatari ya kuvamiwa iwapo taarifa za kuwa na fedha nyumbani zitawafikia watu wenye nia ya uhalifu.
Kwa mujibu wa takwimu za DIB hadi Juni 30, 2026, kulikuwa na zaidi ya akaunti 49.5 milioni za amana katika mabenki, ambapo asilimia 98.98 zilikuwa zinapata kinga ya amana kwa asilimia 100, huku asilimia 1.01 zikipata sehemu ya kinga hiyo.
Amesema tofauti na bima nyingine ambazo zinahitaji mtu kujisajili na kuchangia ada, bima ya amana haitaki mwananchi kulipa ada wala kujisajili moja kwa moja. Mwananchi anachotakiwa kufanya ni kutumia huduma za benki au taasisi ya fedha iliyopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania.
Ameeleza kuwa mfumo huo unalenga kumlinda mwananchi endapo benki au taasisi ya fedha aliyoweka fedha zake itashindwa kuendelea na shughuli zake na kuwekwa chini ya ufilisi.
DIB pia ina jukumu la kusimamia Mfuko wa Bima ya Amana, ambao ulianzishwa mwaka 1994 kwa mchango wa Serikali wa takribani Shilingi bilioni 1.5. Baada ya hapo, mfuko umeendelea kuongezewa fedha kupitia michango ya benki na taasisi za fedha wanachama pamoja na mapato yatokanayo na uwekezaji wa fedha hizo katika hati fungani za Serikali.
Aidha, amesema DIB imepewa jukumu la ziada la kushiriki katika hatua za kuzuia benki au taasisi ya fedha inayokabiliwa na matatizo makubwa kufikia hatua ya kufilisika.
Katika utekelezaji wa jukumu hilo, DIB inaweza kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania kutathmini njia mbalimbali za kuokoa taasisi yenye changamoto, ikiwemo kuunganisha taasisi yenye matatizo na taasisi nyingine, kuuza baadhi ya mali na madeni kwa taasisi nyingine ya fedha au kutoa msaada wa kifedha kwa utaratibu maalum pale inapobainika kuwa hatua hiyo inaweza kupunguza hasara kwenye Mfuko wa Bima ya Amana.
Afisa huyo amesema hatua hizo zinalenga kuhakikisha kuwa amana za wananchi zinalindwa na huduma za kifedha zinaendelea kutolewa, huku ikipunguza uwezekano wa fedha kutoka katika Mfuko wa Bima ya Amana kwa ajili ya kulipa fidia.
Ameeleza kuwa majukumu makuu ya DIB ni pamoja na kukusanya michango ya wanachama, kusimamia Mfuko wa Bima ya Amana, kulipa fidia kwa wateja pale taasisi mwanachama inapofiliskika, kutekeleza majukumu ya ufilisi inapoteuliwa na Benki Kuu ya Tanzania, pamoja na kuchukua hatua za kupunguza hasara kwenye mfuko.
Ametoa wito kwa wananchi kuendelea kutumia huduma za benki na taasisi za fedha zilizopewa leseni na Benki Kuu ya Tanzania, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu kwa usalama wa fedha zao na kuchochea mzunguko wa fedha katika uchumi.
DIB ilianzishwa kwa mujibu wa sheria za sekta ya benki na taasisi za fedha na ilianza rasmi kutekeleza majukumu yake mwaka 1994. Ofisi zake zinapatikana ndani ya Benki Kuu ya Tanzania, Dar es Salaam na Dodoma, huku taarifa zaidi zikipatikana kupitia tovuti ya DIB.




