STAMICO YATWAA TUZO TANO MAONESHO YA TEKNOLOJIA YA MADINI GEITA
GEITA — Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), kupitia Wizara ya Madini, limepokea tuzo tano katika Maonesho ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea mkoani Geita.
Tuzo hizo zimetolewa kwa kutambua mchango wa STAMICO katika shughuli za uchimbaji na maendeleo ya sekta ya madini nchini, huku zikitolewa na wadau mbalimbali, wakiwemo makampuni ya uchorongaji, wachimbaji wadogo wa madini na taasisi zinazojihusisha na shughuli za uchimbaji.
Akizungumza baada ya kupokea tuzo hizo, Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mahusiano ya Umma wa STAMICO, Deus Ntukamazina, amesema kutambuliwa huko ni chachu kwa shirika kuendelea kushirikiana na wachimbaji na wadau wengine wa sekta ya madini.
Amesema STAMICO itaendelea kutoa huduma na ushirikiano kwa wadau wa sekta hiyo, hususan wachimbaji, kwa lengo la kuongeza tija, kukuza shughuli za uchimbaji na kuhakikisha fursa zinazotokana na madini zinawanufaisha Watanzania.
Ntukamazina ameongeza kuwa STAMICO itaendelea kujenga ushirikiano na wadau mbalimbali ili kuchangia ukuaji wa sekta ya madini na kuongeza mchango wake katika uchumi na pato la Taifa.
Tuzo hizo zimepokelewa katika kipindi cha Maonesho ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea Geita, yanayowakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini kwa ajili ya kuonesha teknolojia, huduma na fursa zinazopatikana katika sekta hiyo.




