Breaking News

TBA YATANGAZA FURSA ZA UWEKEZAJI KATIKA MAENEO 38 TANZANIA BARA

GEITA — Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umetangaza fursa mbalimbali za uwekezaji katika maeneo yake 38 yaliyopo Tanzania Bara, ikiwemo mkoani Geita, kwa lengo la kuwawezesha wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kushiriki katika utekelezaji wa miradi kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP).

Akizungumza katika Maonyesho ya Kimataifa ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika Viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mkoani Geita, Meneja wa Mawasiliano na Masoko wa TBA, Adam Mwingira, alisema maonyesho hayo yametumika kama jukwaa la kuwaeleza wadau kuhusu fursa za uwekezaji na huduma zinazotolewa na wakala huo.

Mwingira alisema TBA ina maeneo yaliyotengwa na kuandaliwa kwa ajili ya uwekezaji, hivyo kuwakaribisha wawekezaji kutoka ndani na nje ya nchi kushirikiana na Serikali kupitia mfumo wa PPP.
Kwa upande wa Geita, alisema TBA inaendelea na mipango ya kutekeleza miradi mbalimbali, ikiwemo ujenzi wa majengo ya makazi katika eneo la Mission Quarter, ambapo mradi huo unatarajiwa kuwa na jumla ya apartments 112 katika takribani maghorofa sita.

Aidha, TBA imeendelea kutekeleza miradi ya ujenzi wa majengo ya Serikali na nyumba za viongozi na watumishi wa umma katika maeneo mbalimbali nchini. Miongoni mwa miradi hiyo ni nyumba ya Mkuu wa Mkoa wa Geita, ambayo tayari imekamilika.

Katika sekta ya afya, Mwingira alisema TBA imehusika katika ujenzi wa miundombinu ya hospitali, ikiwemo Hospitali ya Chato na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita, zinazotoa huduma kwa wananchi.
Alisema pia TBA inaendelea na utekelezaji wa miradi ya nyumba za makazi kwa watumishi wa umma, ikiwemo Magomeni Kota, ambapo awamu ya kwanza imekamilika na nyumba zimeanza kutumika, huku awamu ya pili ikiendelea.

Mbali na ujenzi, Mwingira alisema TBA pia hutoa ushauri kwa Serikali katika masuala ya majengo, akitolea mfano Jengo la Ikulu Chamwino, ambalo wakala huo ulihusika katika ubunifu na usimamizi wa ujenzi.
Katika maonyesho hayo, TBA pia imepata nafasi ya pili katika kundi la taasisi za umma, hatua ambayo Mwingira alisema imechangiwa na ushiriki na uungwaji mkono wa wadau waliotembelea banda la wakala huo.

Mwingira amewashukuru wadau kwa ushirikiano wao na kuwataka wananchi na wawekezaji kuendelea kufuatilia taarifa za TBA kupitia vyombo vya habari na mitandao ya kijamii ili kupata taarifa kuhusu fursa za uwekezaji na huduma zinazotolewa na wakala huo.