WABUNIFU 60 WAWANIA NAFASI 20 BORA WA WAZO BUNIFU
DAR ES SALAAM - Mjasiriamali Paschal Christian Emmanuel ni miongoni mwa wabunifu 60 waliofanikiwa kuingia hatua ya fainali ya shindano la Wazo Bunifu, linalolenga kupata mawazo yenye uwezo wa kuboresha huduma na kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.
Emmanuel ni miongoni mwa washiriki wanaofanyiwa mahojiano na Kamati Huru ya Wazo Bunifu katika Hoteli ya Serena jijini Dar es Salaam, ambapo wanapata fursa ya kuwasilisha na kutetea mawazo yao ya ubunifu.
Washiriki hao wamebuni mifumo na suluhisho za kiteknolojia wanazoamini kuwa, zikikubaliwa na kutumiwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zitasaidia kuboresha mifumo ya utendaji kazi, kurahisisha huduma kwa walipakodi na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.
Kupitia mahojiano hayo, Kamati Huru inatathmini mawazo ya washiriki wote 60 kwa kuzingatia ubunifu, uwezo wa kutatua changamoto zilizopo na mchango wake katika kuboresha huduma za TRA.
Mchakato huo unalenga kubaini mawazo 20 bora yatakayopatiwa zawadi, ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha ubunifu na matumizi ya teknolojia katika kuboresha huduma na kuongeza tija katika ukusanyaji wa mapato ya Serikali.




