BoT YAHIMIZA MATUMIZI SAHIHI YA NOTI ZA FEDHA KUEPUSHA GHARAMA ZA ZIADA
Dar es salaam - WANANCHI wameonywa dhidi ya tabia ya kuharibu kwa makusudi sarafu (noti) za Tanzania huku wakikumbushwa umuhimu wa kuzitunza kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa ili kupunguza gharama za uchapishaji na uingizwaji wa fedha mpya.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kutoka Kurugenzi ya Sarafu, Bw. Shadrack Mapunda leo Novemba 6, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akiwasilisha mada kuhusu utambuzi wa alama za usalama katika noti na utunzaji bora wa fedha katika semina ya siku tatu kwa waandishi wa habari za uchumi na masoko ya fedha.
Bw. Mapunda amesema, utunzaji usiofaa wa noti unaofanywa na baadhi ya wananchi unasababisha fedha hizo kuharibika kabla ya kufikia muda wake wa kawaida wa matumizi, hali inayolazimisha Benki Kuu kuzibadilisha mapema na kuongeza gharama za uchapishaji.
Ameeleza tabia ya kukunja noti, kuzibana kwa pini, kuziweka katika mazingira yasiyofaa na kutozihifadhi kwa uangalifu inachangia kuharibika kwa fedha hizo, ambazo zinatarajiwa kudumu kwa takribani mwaka mmoja na nusu.
Pia, aliongeza kuwa gharama zinazotumika kuchapisha noti mpya kutokana na uharibifu unaosababishwa na utunzaji mbaya zingeweza kuelekezwa katika shughuli nyingine za maendeleo ikiwemo ujenzi wa barabara na miundombinu.
Akizungumzia taratibu za kubadilisha noti zilizochakaa au kuharibika, Bw. Mapunda amesema, si kila noti iliyoharibika inastahili kubadilishwa, kwani kuna vigezo maalumu vinavyopaswa kuzingatiwa.
Amesema, miongoni mwa vigezo hivyo ni noti husika kuwa halali na kubaki na angalau asilimia 75 ya ukubwa wake wa awali, huku pande zote mbili za noti yaani mbele na nyuma, zikionekana na kuwezesha kutambulika kwa taarifa na alama zake muhimu.
Bw. Mapunda ameongeza kuwa, noti zilizoharibika kwa kiwango kikubwa, zikiwemo zilizoliwa, kuungua au kufutika kwa alama muhimu za utambuzi zinaweza kushindwa kukidhi vigezo vya kubadilishwa na hivyo kusababisha hasara kwa mmiliki wake.




