MAAFISA WA CHUO CHA TAIFA CHA ULINZI (NDC) WAPIGWA MSASA KUHUSU HISTORIA YA TANZANIA NA HARAKATI ZA UKOMBOZI WA AFRIKA
DAR ES SALAAM - Chuo cha Taifa cha Ulinzi (National Defence College- Tanzania) kimeongeza maarifa kuhusu historia ya Tanzania na harakati za ukombozi wa Bara la Afrika.
Sambamba na kutambua mchango wa urithi na malikale katika kukuza uchumi wa Taifa, kupitia ziara ya kielimu iliyofanyika katika Makumbusho na Nyumba ya Utamaduni, Posta, jijini Dar es Salaam.
Ujumbe wa Chuo hicho, ukiongozwa na Mkuu wa Chuo, Balozi Meja Jenerali Wilbert Augustin Ibuge umepokelewa na Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt. Noel Biseko Lwoga, pamoja na Menejimenti ya Makumbusho.
Ziara hiyo imelenga kuwawezesha washiriki kujifunza historia ya Tanzania na harakati za ukombozi wa Bara la Afrika, kwa kuzingatia mchango wa viongozi, matukio na juhudi mbalimbali zilizochangia kupatikana kwa uhuru na kujenga misingi ya umoja na mshikamano wa Mataifa ya Afrika.
"Ziara hii ni chachu ya kuonyesha namna urithi wa taifa unavyohifadhiwa, unavyotangazwa na kuhamasisha jamii," amesema Dkt. Lwoga.
Aidha, ziara hiyo imewapa washiriki fursa ya kutambua umuhimu wa urithi wa Taifa na malikale katika kukuza uchumi, hususan kupitia uhifadhi, utalii wa urithi, utoaji wa elimu na matumizi endelevu ya rasilimali za urithi kwa maendeleo ya Taifa.
Kupitia ziara hiyo, washiriki wameongeza uelewa kuhusu nafasi ya Makumbusho katika kuhifadhi na kuwasilisha historia ya Taifa, kuimarisha uzalendo na utambulisho wa Taifa, pamoja na kuchochea fursa za kiuchumi zinazotokana na urithi wa kihistoria na kiutamaduni.
Ziara hiyo inaonesha umuhimu wa ushirikiano baina ya taasisi katika kuendeleza elimu ya historia, urithi wa utamaduni na malikale, sambamba na kuimarisha uelewa wa mchango wake katika maendeleo ya Taifa.
Makumbusho ya Taifa la Tanzania yaendelea kutekeleza jukumu lake la kukusanya, kutafiti, kuhifadhi, kutoa elimu na kutangaza urithi wa Taifa, kwa lengo la kuhakikisha historia na utamaduni wa Tanzania vinaendelea kuwa chachu ya uzalendo, maarifa na maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa vizazi vya sasa na vijavyo.







