Breaking News

CHALAMILA KUZINDUA KAMPENI YA DAR ES SALAAM SAFI, ATOA WITO WA USHIRIKIANO

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, ametangaza kuzindua kampeni maalumu ya usafi wa jiji itakayokwenda sambamba na utoaji huduma mbalimbali ikiwemo kuwasaidia wanafunzi wa chuo waliokosa mkopo.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Chalamila amesema kampeni hiyo itatumia kaulimbiu isemayo Dar es Salaam Safi Inatokana na Ushiriki wa Pamoja, ikiwa na lengo la kuhamasisha wananchi kujenga utamaduni wa kutunza mazingira na kuhakikisha jiji linakuwa safi wakati wote.

Amesema kampeni hiyo itazinduliwa rasmi Novemba 14,2026, katika Viwanja vya Posta jijini Dar es Salaam, kuanzia asubuhi, ambapo shughuli mbalimbali zitafanyika ikiwemo zoezi la usafi, uhamasishaji wa matumizi sahihi ya vifaa vya usafi na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kutunza mazingira.

Chalamila amesema katika kampeni hiyo wadau mbalimbali wamejitokeza kushirikiana na mkoa, wakiwemo makampuni yanayotengeneza na kusambaza vifaa vya usafi, huku akiwataka wananchi, taasisi na wafanyabiashara kuunga mkono juhudi hizo kwa vitendo ili kufanikisha lengo la kuwa na jiji safi.

Amebainisha kuwa Dar es Salaam inazalisha takribani tani 4,657 za taka kwa siku, lakini zaidi ya asilimia 60 pekee ndizo zinazofikishwa katika dampo, huku takribani asilimia 40 zikibaki mitaani, kwenye mifereji na mito, hali inayochangia uchafuzi wa mazingira na kuziba kwa mifumo ya maji.

Alisema hali hiyo inahitaji hatua za pamoja za kukabiliana na changamoto ya taka, akieleza kuwa mkoa umepata mwekezaji kutoka Ghana ambaye amewekeza katika dampo la Pugu kwa ajili ya kuboresha shughuli za utunzaji na uchakataji wa taka, hatua inayotarajiwa kuongeza ufanisi katika usimamizi wa taka zinazozalishwa jijini.

Katika hatua nyingine, Chalamila amesema kampeni hiyo itakuwa na huduma mbalimbali za kijamii, ikiwemo kliniki ya sheria itakayowapa wananchi fursa ya kupata ushauri kuhusu masuala ya kisheria, pamoja na kuwasaidia wafanyabiashara wadogo na vijana wanaokabiliwa na changamoto za mikopo kupata elimu na mwongozo wa namna ya kunufaika na fursa zilizopo.