GST KUFANYA UTAFITI WA ENEO LA EKARI 157,192 KUBAINI MWENDELEZO WA MKONDO WA MADINI YA TANZANITE
# Lengo ni kuongeza uzalishaji wa madini ya Tanzanite
# Utafiti kugusa eneo la nje ya ukuta wa eneo tengefu la Mirerani
# Wachimbaji wa Mirerani wamshukuru Rais Samia kwa mkakati wa kukuza biashara ya Madini
# GST yaelekezwa kukamilisha utafiti eneo la Lemshuku kuongeza uzalishaji wa Green Garnet
Mirerani, Manyara - Serikali kupitia Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imezindua rasmi mpango wa kufanya utafiti wa kina wa kijiolojia kwa kutumia teknolojia za kisasa, zikiwemo ndege maalumu zisizo na rubani (Drone), ndege za utafiti zinazoruka karibu na uso wa dunia pamoja na vifaa vingine vya kisasa, kwa lengo la kubaini maeneo yenye viashiria vya uwepo wa madini nchini.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Peter Mavunde, wakati wa hafla ya uzinduzi wa utafiti wa kubaini mwendelezo wa mkondo wenye madini ya Tanzanite katika eneo tengefu la Mirerani, iliyofanyika leo Novemba 09, 2026.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Mavunde amesema kuwa hadi sasa ni asilimia 16 pekee ya eneo la Tanzania lililofanyiwa utafiti wa kina wa kijiolojia, huku asilimia 84 iliyobaki, sawa na takribani ekari milioni 233, ikiwa bado haijafanyiwa utafiti wa kina.
Ameeleza kuwa katika hatua ya kuongeza wigo wa tafiti hizo, Serikali inatarajia kufanya utafiti katika eneo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 160,772, sawa na asilimia 18 ya eneo la nchi, kupitia ushirikiano na wataalamu kutoka Hispania. Maeneo mengine yatakayofanyiwa utafiti ni Kigoma, Rukwa, Katavi, Mbeya, Songwe, Lindi na Mtwara, huku utafiti mwingine ukihusisha maeneo ya Dodoma, Singida, Tabora hadi Shinyanga.
Aidha, Mhe. Mavunde amesisitiza kuwa Serikali imeanza kutenga asilimia 10 ya mapato yanayokusanywa katika sekta ya madini kwa ajili ya kugharamia tafiti za kina za kijiolojia. Hatua hiyo inalenga kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata taarifa sahihi kuhusu maeneo yenye madini na kupunguza uchimbaji wa kubahatisha unaosababisha upotevu wa muda na mitaji.
Naye, Mtendaji Mkuu wa GST, Mhandisi Ally Samaje, amesema kuwa lengo kuu la utafiti huo ni kuongeza uzalishaji wa madini









