Breaking News

MAWAKILI WA SERIKALI WATAKIWA KULINDA UTAWALA WA SHERIA, HAKI ZA RAIA NA KUWA WAADILIFU

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Katiba na Sheria Balozi Baraka Haran Luvanda, amewataka Mawakili wa Serikali nchini kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na uwajibikaji ili kuhakikisha utawala wa sheria unazingatiwa na haki za wananchi zinalindwa.

Akizungumza jijini Dodoma Novemba 16, 2026 katika Ufunguzi wa Kikao Kazi cha Viongozi wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) kilichofanyika katika Ofisi za Wizara ya Katiba na Sheria, Mji wa Serikali Mtumba.

Balozi Luvanda amesema mawakili hao wana nafasi kubwa katika jamii kwa kuwa ni sehemu muhimu ya kusimamia haki na kuhakikisha misingi ya utawala wa sheria inazingatiwa kwa sababu wao ni maaskari wa Kalamu wanaotumia kalamu kulinda utawala wa sheria na haki za raia.
Amesisitiza kuwa, ili chama hicho kiweze kuwa imara na kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, kinapaswa kuimarisha ushirikiano miongoni mwa wanachama, kuongeza muonekano wake katika jamii pamoja na kubuni vyanzo endelevu vya mapato vitakavyokiwezesha chama hicho kujiendesha. 

Aidha, amehimiza uwekezaji katika mafunzo na kuwajengea uwezo wanachama kupitia elimu endelevu ya sheria.

Kwa upande wake, Rais wa TPBA, Bw. Bonaventure Pardon Mwambaja, amesema chama hicho kimepokea maelekezo na ushauri wa mgeni rasmi na kipo tayari kuyafanyia kazi ili kuimarisha utendaji, mshikamano na maendeleo ya chama.
Naye Mwenyekiti wa TPBA, Bi. Selestina Kunambi, amesema mawakili wa Serikali wataendelea kutekeleza wajibu wao kwa kuzingatia misingi ya taaluma ya sheria, huku akieleza kuwa ushauri uliotolewa na mgeni rasmi ni muhimu katika kuimarisha utendaji wa chama na wanachama wake.

Vilevile, Katibu wa TPBA, Bw. Salmin Zuberi, amesema chama kitaendelea kuweka mikakati ya kukijenga na kukiimarisha ili kiweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kikao Kazi hicho kilichoanza Novemba 16, 2026, kimewakutanisha viongozi na wawakilishi wa chama kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara kwa lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu uimarishaji wa chama, ushirikiano wa wanachama na maendeleo ya taaluma ya uwakili wa Serikali nchini. Kikao hicho kinatarajiwa kuhitimishwa Novemba 18, 2026