Breaking News

TANZANIA YAPATA FURSA ZA UWEKEZAJI WA DOLA BILIONI 4.7 KUPITIA COP31

# Fedha hizo zitaimarisha nishati safi, uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi

NA Mwandishi Wetu, Dar es Salaam - Tanzania imepata ahadi na fursa za uwekezaji zenye thamani ya takribani dola za Marekani bilioni 4.7 kupitia Mkutano wa 31 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (COP31), uliofanyika Antalya, Uturuki, kuanzia Novemba 20, mwaka huu.

Fedha hizo zinatarajiwa kuelekezwa katika miradi mbalimbali ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, ikiwemo nishati safi ya kupikia, nishati jadidifu, uhifadhi wa mifumo ya ikolojia, ulinzi wa jamii zilizo katika hatari ya athari za tabianchi pamoja na kuimarisha uchumi wa kijani.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana kutokana na ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo.

Alisema mafanikio hayo yametokana na ushiriki wa Tanzania uliojikita katika kaulimbiu ya kitaifa isemayo Hatua Jumuishi za Tanzania za Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi kwa Ajili ya Dira ya 2050: Kujenga Taifa Imara la Kijani na Lenye Ustawi.

Alisema kaulimbiu hiyo ililenga kusisitiza umuhimu wa kuhusisha makundi yote ya jamii katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kujenga ustahimilivu wa taifa, kuimarisha uchumi wa kijani na kuhakikisha ustawi wa wananchi.

Masauni alisema ushiriki wa Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano huo ulikuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha nafasi ya Tanzania kimataifa na kufungua fursa mbalimbali za ushirikiano na uwekezaji.

Alisema Rais Samia katika hotuba yake aliyotoa Novemba 11, mwaka huu, alisisitiza vipaumbele vitatu ambavyo ni upatikanaji wa fedha za kutosha na zenye masharti nafuu za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, kuimarisha mpito wa haki wa nishati na kuendeleza maendeleo jumuishi kupitia teknolojia, ubunifu na ajira za kijani kwa kuzingatia Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.

Akizungumzia mafanikio katika eneo la fedha, Masauni alisema Benki ya Maendeleo ya Afrika imeidhinisha ufadhili wa ununuzi wa majiko 70,000 ya kisasa yanayotumia umeme kwa ajili ya shule na vituo vya afya, yenye thamani ya dola milioni 54.

Alisema majiko mengine 70,000 yenye thamani sawa na hiyo yanatarajiwa kuidhinishwa kupitia mradi mwingine wa nishati unaofadhiliwa na benki hiyo.

Aidha, taasisi ya Sustainable Energy for All (SEforALL) imeahidi kuijumuisha Tanzania katika mpango wa uwekezaji unaozidi dola bilioni nne kwa ajili ya kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia na kusaidia nchi kuwa kitovu cha uzalishaji wa majiko na teknolojia husika.

Alisema Serikali ya Uingereza kupitia UK Aid imeahidi pauni milioni mbili, sawa na dola milioni 2.6, kwa ajili ya nishati safi ya kupikia na pauni nyingine milioni mbili kwa nishati jadidifu.

Kupitia mpango huo, wananchi milioni moja wanatarajiwa kunufaika kwa kupata majiko ya umeme na kulipia gharama zake kidogo kidogo kupitia bili za umeme.

Masauni aliongeza kuwa mfuko wa Green Climate Fund (GCF) umeahidi dola milioni sita kwa ajili ya kuimarisha uwezo wa nchi kuandaa na kutekeleza miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Alisema Tanzania pia imepata mafanikio baada ya Baraza la Taifa la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (NEMC) kupata ithibati ya GCF, hatua inayoiwezesha taasisi hiyo kupata fedha za moja kwa moja kwa ajili ya miradi ya mazingira.

Alisema kwa sasa Tanzania ina taasisi mbili zenye ithibati ya mfuko huo ambazo ni NEMC na Benki ya CRDB, huku Wizara ya Fedha ikiwa katika hatua za mwisho za kupata ithibati hiyo.

Katika hatua nyingine, alisema Mfuko wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu (Loss and Damage Fund) umeidhinisha hatua za upatikanaji wa dola milioni 20 kupitia CRDB kwa ajili ya miradi itakayosaidia jamii zilizoathirika na mabadiliko ya tabianchi katika maeneo ya visiwa vidogo, pwani na kanda za maziwa, hususan Zanzibar, Kigoma na Pwani.

Alisema Benki ya Maendeleo ya Afrika pia imeahidi dola milioni 26 kwa ajili ya miradi ya kuhifadhi mifumo ya ikolojia ya bahari na kuimarisha ustahimilivu wa jamii.

Masauni alitaja mafanikio mengine kuwa ni pamoja na ahadi ya Saudi Arabia kuendelea kufadhili miradi ya nishati jadidifu na nishati safi ya kupikia, huku kampuni ya App Energy ikiahidi kuendeleza miradi ya nishati safi ya kupikia katika shule 3,000 kwa uwekezaji wa takribani dola milioni 30 kupitia ushirikiano wa Tanzania na Japan katika biashara ya kaboni.

Alisema pia International Solar Alliance imejumuisha Tanzania katika mpango wa uwekezaji wa dola milioni 200, huku US-China Green Fund ikiweka mpango wa kusaidia nchi zinazoendelea katika eneo la nishati safi ya kupikia wenye thamani ya dola milioni tatu.

Akizungumzia usimamizi wa fedha hizo, Masauni alisema serikali itafuatilia kwa karibu ahadi zote ili kuhakikisha fedha zinafika nchini, zinaelekezwa katika shughuli zilizokusudiwa na kusimamiwa kwa uwazi na uwajibikaji.

MIKATABA YA USHIRIKIANO

Katika eneo la ushirikiano wa kimataifa, alisema Tanzania imesaini hati ya makubaliano na Sekretarieti ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) ili kuwa mwenyeji wa mikutano ya masuala ya tabianchi.

Alisema hatua hiyo inaiweka Tanzania katika nafasi ya kuwa nchi ya pili duniani kufanya hivyo na inatarajiwa kuimarisha diplomasia ya mazingira pamoja na kukuza utalii wa mikutano.

Masauni alisema kupitia makubaliano hayo, Tanzania inajiandaa kuwa mwenyeji wa mikutano miwili ya UNFCCC mwaka 2027, ikiwemo mkutano unaotarajiwa kufanyika Februari.

Aidha, Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Kituo cha Kuratibu Biashara ya Kaboni (SCMC) imesaini hati za makubaliano na taasisi mbalimbali za kimataifa kwa lengo la kuimarisha usimamizi wa masoko ya kaboni, usajili wa miradi, uidhinishaji na utoaji wa mikopo ya kaboni inayokidhi viwango vya kimataifa.

Alizitaja taasisi hizo kuwa ni International Emissions Trading Association (IETA), Era City UG na Verra.

TANZANIA MWENYEJI WA KITUO CHA VIJANA AFRIKA

Katika mafanikio mengine, Masauni alisema Tanzania imepata uthibitisho rasmi wa kuwa mwenyeji wa Kituo cha Majadiliano ya Vijana kuhusu Tabianchi kwa Bara la Afrika (African Youth Negotiators Center).

Alisema kituo hicho kitakuwa na jukumu la kujenga uwezo wa vijana wa Afrika kushiriki katika majadiliano ya kimataifa kuhusu mabadiliko ya tabianchi.

Alisema hatua hiyo imekuja baada ya wazo hilo kupendekezwa na Umoja wa Afrika na baadaye kuidhinishwa katika mkutano wa wataalamu na watendaji wakuu wa nchi za Afrika.

Pia, alisema Mtanzania Upendo Limo, mwanafunzi wa shahada ya uzamivu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ametunukiwa tuzo ya kwanza ya UN Climate Change AI Global Award 2026 kutokana na ubunifu wa matumizi ya akili unde katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Masauni alisema mafanikio mengine ni Zanzibar kutambuliwa kuwa Jiji Lisilo na Taka (Zero Waste City) na kuchaguliwa kuwa miongoni mwa maeneo 20 ya awali kutoka nchi 11 duniani yatakayotekeleza mpango wa kimataifa wa maeneo yasiyo na taka.

MAAZIMIO YA MKUTANO

Akizungumzia maazimio ya mkutano huo, Masauni alisema nchi wanachama zimekubaliana kuendeleza mpango wa miaka mitatu wa kuimarisha matumizi ya nishati safi kwa kuzingatia mazingira na mahitaji ya maendeleo ya kila nchi.

Alisema mpango huo unalenga kuimarisha ushirikiano, upatikanaji wa wataalamu na kujenga uwezo wa nchi katika kutekeleza mpito wa haki wa nishati.

Alisema Tanzania itasisitiza kuwa mabadiliko ya matumizi ya nishati yazingatie upatikanaji wa nishati ya uhakika, ajira, haki za wananchi, teknolojia na mahitaji ya maendeleo ya taifa.

Aliongeza kuwa Tanzania inalenga kuhakikisha ifikapo mwaka 2034, asilimia 80 ya wananchi wanatumia nishati safi ya kupikia.

Katika eneo la kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, alisema nchi zimekubaliana kukamilisha viashiria vitakavyotumika kupima hatua zinazochukuliwa na mataifa katika kukabiliana na athari kama ukame, mafuriko na kupanda kwa kina cha bahari.

Mwongozo wa viashiria hivyo unatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 2027, hatua itakayosaidia kupima ufanisi wa miradi na matumizi ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Kuhusu Mfuko wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi, alisema nchi zimekubaliana mfuko huo kupata asilimia tano ya mapato yatokanayo na biashara ya kaboni chini ya Makubaliano ya Paris.

Alisema pia nchi zimeahidi jumla ya dola milioni 50.2 kwa ajili ya kuongeza fedha katika mfuko huo, huku Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi zinazonufaika.

Alisema hadi sasa miradi sita yenye thamani ya takribani dola milioni 9.9 imeidhinishwa kwa Tanzania, ikiwemo mradi mpya wa dola milioni nne wa kurejesha ikolojia ya Ziwa Babati kwa lengo la kuimarisha kilimo na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabianchi katika Wilaya ya Babati.

Masauni alisema nchi wanachama pia zimekubaliana kuimarisha taratibu za biashara ya kaboni, ikiwemo usimamizi wa mauzo na ununuzi wa viwango vya kaboni, kujenga mifumo ya usimamizi na kuongeza ujuzi wa wataalamu.

Alisema hatua hiyo itaiwezesha Tanzania kutumia fursa za biashara ya kaboni kwa uwazi na kuhakikisha wananchi wananufaika na miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.

Katika sekta ya kilimo na usalama wa chakula, alisema nchi zimekubaliana kuimarisha utafiti, upatikanaji wa taarifa za kisayansi na teknolojia zitakazosaidia wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Alisema ushirikiano huo utasaidia wakulima kupata taarifa sahihi za hali ya hewa, kutumia mbinu za kilimo zinazohimili ukame na mafuriko, kuongeza uzalishaji na kuimarisha usalama wa chakula.

Hata hivyo, Masauni alisema pamoja na mafanikio hayo, mkutano huo haukuafikiana katika baadhi ya masuala muhimu yaliyokuwa yakijadiliwa, kutokana na tofauti za misimamo ya nchi wanachama kuhusu lugha na namna ya kushughulikia baadhi ya masuala ya mabadiliko ya tabianchi.

Alisema baadhi ya majadiliano hayo yameongezewa muda na yataendelea katika mikutano ijayo, ikiwemo COP32 itakayofanyika Addis Ababa, Ethiopia.

Alisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa ndani na wa kimataifa kuhakikisha fursa zilizopatikana kupitia COP31 zinageuzwa kuwa miradi halisi yenye manufaa kwa wananchi na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.