SERIKALI KUENDELEA KUTOA DAWA BURE KWA WAGONJWA WA UKIMWI NA KIFUA KIKUU
Serikali kupitia Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuwa sera yake ya
kutoa dawa bure kwa wagonjwa wa kifua kikuu, ukimwi, mama wajawazito,
wazee na watoto chini ya miaka mitano inaendelea.
Hayo yamesemwa leo, mjini Dodoma
na waziri wa wizara hiyo Mhe. Ummy Mwalimu alipokuwa akitolea ufafanuzi
wa swali la Mbunge wa Chalinze Mhe. Ridhiwani kikwete juu ya taarifa
zilizotolewa na vyombo vya habari kuwa utoaji wa dawa bure kwa makundi
hayo ya watu umesitishwa na wanatakiwa kulipia.
“Hakuna mabadiliko yoyote katika
sera ya kutoa dawa bure kwa wagonjwa wa ukimwi, kifua kikuu, mama
wajawazito, wazee na watoto chini ya miaka mitano, aidha nitaitaka
hospitali ya Taifa ya Muhimbili inipatie maelezo juu ya taarifa hizo,”
alisisitiza, Mhe. Ummy.
Wakati huo huo, naibu waziri wa
wizara hiyo, Mhe. Dkt. Hamisi Kigwangalla amesema kuwa wizara hiyo kwa
kushirikiana na wizara ya Biashara, Viwanda na Uwekezaji wanaandaa
mkakati wa kuongeza uzalishaji wa dawa nchini ili angalau kukidhi
asilimia 60 ya mahitaji katika kipindi cha miaka mitano ijayo.
Aidha wizara hiyo pia iko katika
mikakati ya kuunda chombo cha kusimamia gharama na bei zinazotozwa na
vituo vya kutolea huduma za afya ikiwa pamoja na bei za dawa na vifaa
tiba ili kuthibiti uongezaji holela wa bei za dawa na vifaa tiba.



