KUTOKA BASATA;WIMBO WA ‘PALE KATI PATAMU’ WA NEY WA MITEGO WAFUNGIWA NA KUPIGWA MARUFUKU
Msanii Emmanuel Elibariki (Ney Wa Mitego)
Baraza
la Sanaa la Taifa (BASATA) limeufungia rasmi wimbo wa ‘pale kati
patamu’ ulioimbwa na Msanii Ney wa Mitengo kutokana na ukiukwaji mkubwa
wa maadili.
Msanii huyu amekuwa na tabia na
mienendo yenye kuchafua Sekta ya Sanaa yeye binafsi kupitia kutoa kazi
chafu na kufanya maonesho yenye kukiuka maadili. Kazi zake zikikiuka
maadili na kudhalilisha utu wa mwanamke sambamba na kutoa lugha za
matusi na za kudhalilisha watu wa kada mbalimbali.
Ieleweke kwamba kwa mujibu wa
kifungu namba 4(L) cha Sheria ya BASATA namba 23 ya mwaka 1984, Baraza
limepewa jukumu la kuhakikisha linalinda maadili miongoni mwa wasanii
wanapokuwa jukwaani au wanapobuni kazi yoyote ya sanaa.
ikumbukwe kwamba BASATA
limeshamuita na kumuonya msanii huyu mara kadhaa kutokana na tabia yake
ya kutoa kazi zisizokuwa na maadili na aliahidi kubadilika na kuachana
na tabia hiyo. Kwa hiyo kuendelea kwake kufanya matukio haya kwa
makusudi ni uthibitisho kwamba hajabadilika na kwa maana hiyo ameendelea
kuidhalilisha Sanaa na wasanii wa kitanzania wenye kujitambua na
kuiheshimu kazi ya sanaa kama kazi nyingine. Kwa sasa Msanii huyu ametoa
wimbo mwingine wa Pale Kati patamu ambao uko mitandaoni ukipambwa na
picha chafu zinazoonesha mwanamke akiwa mtupu yaani uchi wa mnyama.
Kwa mantiki hii BASATA
halitavumilia wasanii wachache ambao wanataka kuigeuza tasnia ya sanaa
na wasanii genge la wahuni wasio na staha na wanaojipanga kuibomoa
jamii. BASATA linapenda kueleza ya kufuatayo
· BASATA linatamka kuwa limeufungia wimbo huu rasmi kutumika kwa namna yoyote ile.
· Aidha pamoja na adhabu ya kufungia wimbo huu hatua nyingine za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Aidha, BASATA linawataka Wasanii wote nchini kufuata sheria, kanuni na taratibu mara wanapotengeneza kazi zao.
SANAA NI KAZI, TUIKUZE, TUILINDE NA KUITHAMINI
Godfrey Mngereza
KATIBU MTENDAJI



