Washiriki wa
Mtandao wa Wanataaluma wa Vyuo Vikuu Vinavyotoa Mafunzo yahusuyo Usimamizi wa
Ardhi Kanda ya Afrika Mashariki kutoka
nchi 9 za Bara la Afrika wakifuatilia Mkutano wa mtandao huo leo jijini Dar es
salaam.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu
Ardhi Prof. Idrissa Mshoro akizungumza na waandishi wa Habari leo jijini Dar es
salaam mara baada ya Ufunguzi wa Mkutano wa Wanataaluma ya Usimamizi wa Ardhi
Kanda ya Afrika Mashariki .
Katibu Mkuu
wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Mozes Kusiluka
akiwaeleza waandishi wa Habari kuhusu mpango wa Serikali wa kupima na
kurasimisha maeneo yasiyopimwa katika jiji la Dar es salaam leo.
Na. Aron Msigwa –MAELEZO.
Serikali imewataka wataalam wa vyuo Vikuu vinavyotoa mafunzo ya
Usimamizi wa Ardhi waitumie taaluma yao katika kutafuta suluhisho la migogoro
ya Ardhi inayowakumba wananchi katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizungumza kwa Niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na
Mafunzo ya Ufundi wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Wanataaluma ya Usimamizi wa
Ardhi Kanda ya Afrika Mashariki leo jijini Dar es salaam, Naibu Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo (Sayansi) Prof. Simon Msanjila amesema kuwa wataalam hao wanalo
jukumu la kufuatilia migogoro inayotokea nchini na kuhakikisha wanatoa ushauri
wa kitaalam utakaotoa majibu ya utatuzi wa migogoro hiyo.
“Ninyi kama watalaam wa sekta ya Ardhi lazima mtoe majibu kwa nini
migogoro ya ardhi inaendelea kutokea katika maeneo mbalimbali licha kuwepo kwa
kanuni, Sheria na taratibu zinazosimamia sekta ya Ardhi nchini” Amesema
Prof.Msanjila.
Ameeleza kuwa wao kama watalaam wa sekta hiyo wanatakiwa kwenda
zaidi kwenye matatizo halisi na kuwawafikia wananchi wengi zaidi kwa
kushirikiana na wadau mbalimbali ili kuondoa
changamoto zao kuliko kucheza na vitabu na kuongea kwenye Ofisi.
Amewataka wataalam hao hasa
wale walioko nchini Tanzania kufika katika maeneo yenye migogoro ya Ardhi
ikiwemo Morogoro na maeneo mengine ili kuangalia kwa nini wananchi wanaendelea
na mapigano tunajua ipo migogoro ya Ardhi inayotokea katika mikoa ya Morogoro,
Pwani na mikoa mingine,
Amesema kuwa kwa upande wa Serikali suala la ufumbuzi wa migogoro
ya Ardhi linaendelea kupewa kipaumbele kwa kuhakikisha kuwa ardhi inaendelea
kutolewa kwa kuzingatia sheria pia kushughulikia changamoto zote zinazokwamisha
ustawi wa sekta ya ardhi hususan uondoaji kero zote zinazokwamisha matumizi
bora ya ardhi kwa jamii.
Akifafanua kuhusu nafasi ya Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia
na Mafunzo ya Ufundi katika mkutano huo ameeleza kwamba kupitia mkutano huo wa
kitaalam wa masuala ya Ardhi, Wizara hiyo inajifunza kuhusu changamoto zitakazojitokeza na kuibuliwa ili ziwekwe
kwenye mitaala kwa lengo la kuwaandaa watalaam watakaokuwa na uwezo wa
kusuluhisha matatizo yote yanayojitokeza kwenye sekta hiyo.
Amesema kuwa Sekta ya Elimu kupitia mkutano huo itaboreshwa kwa
kupata nyongeza ya utalaam kutoka kwa wataalam kutoka Vyuo vikuu vya nchi
mbalimbali za Bara la Afrika waliohudhuria mkutano huo na kuongeza kuwa Chuo
Kikuu Ardhi nchini Tanzania ambacho kimebobea kwenye masuala ya Ardhi kitapata
taarifa zaidi katika uboreshaji wa mitaala na mafunzo ya Programu za Utawala wa
Ardhi, Ugawaji wa Ardhi na Upimaji wa Ardhi”
Kwa Upande wake Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Ardhi Prof. Idrissa
Mshoro akizungumza mara baada katika mkutano huo amesema kuwa wataalam wa Ardhi
nchini Tanzania bado wana umuhimu mkubwa katika maendeleo ya sekta ya Ardhi na
kufafanua kuwa wao kama chuo kinachozalisha watalaam wa Ardhi wanalo jukumu kuzalisha
watalaam watakaofanya usimamizi thabiti wa Ardhi kukabiliana na changamoto
zilizopo.
“Sisi nafasi yetu kama Chuo Kikuu Ardhi ni kujua ni namna gani
tunavyoweza kuzalisha wataalam wa kutosha wenye weledi watakaoweza kukabiliana
na changamoto mbalimbali zilizoko kwenye sekta ya Ardhi pia kuhakikisha
wataalam tunaozalisha wanakidhi ubora na matarajio ya wananchi” Amesema Prof.
Mshoro.
Amesema kuwa wanataaluma kutoka Tanzania watanufaika kutokana na mkutano
huo kwa kuwa unawajumuisha watalaam wa Ardhi kutoka takribani nchi 9 watakaobadilishana
uzoefu kuhusu changamoto mbalimbali za ardhi zinazojitokeza katika maeneo yao
na namna wanavyozitatua.
Aidha, amesema kuwa Sekta ya Ardhi nchini Tanzania bado
inakabiliwa na uhaba wa watalaam wa kutosha
ambao wangeweza kusimamia maamuzi katika masuala ya Ardhi ngazi za chini
na kuongeza kuwa ili kupata maamuzi na taarifa sahihi za ardhi ni lazima suala
la uwepo wa watalaam hao liendelee kupewa kipaumbele.
Kuhusu mchango wa watalaam hao katika utatuzi wa migogoro ya Ardhi
amesema kuwa ipo haja ya watalaam waliopo kutumika ipasavyo kutatua migogoro
inayojitokeza na kuwaletea manufaa wananchi ambao wanahitaji huduma za wataalam
hao.
Mkutano huo unaohusisha Mtandao wa vyuo Vikuu Huo ni mkutano wa
nane nane wa mwake
Amesema kuwa tayari kwa upande wa Serikali tayari watalaam wa
sekta husika wamejipanga kuhakikisha kuwa wanapata suluhisho la mgogoro
inayojitokeza kupitia sheria zilizopo.