WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI WATEKELEZA AGIZO LA RAIS KWA KUCHANGIA MADAWATI.
Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga
(kushoto) akimkabidhi hundi Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa wakati wa
hafla ya makabidhiano madawati ikiwa ni fedha zilizochangwa na
watumishi wa wizara hiyo ikiwa sehemu ya kutekeleza agizo la Rais Mhe. John
Magufuli mapema hii leo katika shule ya Msingi Chamanzi iliyopo wilaya ya
Temeke jijini Dar es Salaam.
Na
Beatrice Lyimo-MAELEZO
Watumishi wa Wizara ya Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wamechangia kiasi cha Tsh. Milioni 100 ikiwa
ni sehemu ya kuhamasisha umma kuhusu zoezi la upatikanaji wa madawati katika
shule za msingi na Sekondari nchini.
Akikabidhi mchango huo kwa Waziri
Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kwa niaba ya watumishi wa wizara hiyo, Waziri wa
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Augustine Mahiga
amesema kuwa watumishi hao wametoa fedha hizo kwa shule ya msingi Chamazi ikiwa
ni utekelezaji wa agizo la Rais la upatikanaji wa madawati katika shule za
msingi na sekondari nchini.
Balozi Mahiga amesema Wizara yake
iliwahamasisha watumishi wake walio makao makuu na wale walio kwenye balozi
mbalimbali nje ya nchi kuchangia zoezi hilo la upatikanaji wa madawati.
“Ili kufanisha upatikanaji wa fedha
hizi Wizara yangu iliwahamasisha watumishi wake wote walio Makao makuu na wale
walio katika balozi zetu duniani kote, wito huu uliitikiwa kwa ari na
hamasa kubwa na kufanikisha kukusanya kiasi cha Shilingi 100,176,825.52 za
kitanzania”alisisitiza Balozi Mahiga
Waziri Mahiga aliongeza kuwa mara
baada ya kukusanya fedha hizo watumishi wa Wizara hiyo waliamua kumpatia
aliyekuwa Mtumishi wa Wizara ambaye sasa ameteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya
Manyoni kiasi cha shilingi Milioni 15 kwa ajili ya ununuzi wa madawati katika
Wilaya yake.
Aidha, amesema kiasi fedha
zilizobaki zaidi ya shilingi milioni 85 zilikabidhiwa kwa Waziri Mkuu wa
Tanzania, Mhe Kassim Majaliwa kwa ajili ya mchango wa utengenezaji wa
madawati ya shule ya Msingi Chamazi iliyoko Wilaya ya Temeke Jijini Dar es
Salaam.
Waziri Mahiga aliongeza kuwa mbali
na wizara yake kuwa na majukumu mbalimbali bado inalo jukumu la kuhakikisha
inaitangaza Tanzania ili kuvutia wawekezaji na kukuza uchumi wa nchi, na
kuongeza kuwa elimu bora ni msingi imara katika kufanikisha hilo.




