Video : TUNDU LISSU ALIVYOSHEREHEKEA MIAKA 20 YA NDOA AKIWA KITANDANI NAIROBI
Utafanya kitu gani ukitimiza miaka 20
ya ndoa? Au ulifanya nini ulipotimiza miaka hiyo ya ndoa?
Kuna ambao hutumia
siku ya kumbukumbu ya ndoa zao kwenda kwenye nyumba za ibada kumshukuru Mungu
na wengine hufanya sherehe kwa kualika ndugu, marafiki na majirani.
Kila mmoja huwa na
utaratibu wake ambao huambatana na uwezo wa kiuchumi ili kuiweka kumbukumbu
hiyo ya ndoa vizuri na ndio maana kuna ambao hufanya sherehe kubwa na wengine
hukumbuka kwa ‘maneno tu’.
Iwe ni kumbukumbu ya
miaka mitano, 10 au 15, huwa ni muhimu kutafakari muunganiko wa watu wawili
ambao wameishi pamoja wakipita milima, mabonde na kuvuka vihunzi vingi.
Iwe ni kwa sherehe au
‘maneno makavu’ tu, siku hiyo huwa ni muhimu kuitafakari na ikiwezekana wawili
hao, huwa wanatathmini walikotoka na wanakokwenda.
Lakini, mbunge wa
Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na mkewe Alicia, wana stori tofauti
kuhusu kumbukumbu ya ndoa yao.
Leo Jumatano, Novemba
29, Lissu na Alicia wanatimiza miaka 20 ya ndoa yao, lakini wanatafakari safari
hiyo ndefu ya muunganiko wao wakiwa mazingira tofauti;Hospitali ya Nairobi.
Wanaweza kuitumia
siku ya leo kulishana keki, lakini Lissu anatimiza siku 84 akiwa Hospitali ya
Nairobi huku mkewe, Alicia akiwa kando ya kitanda kumhudumia kwa siku zote
hizo.
Lissu aliyepigwa risasi
zaidi ya 30 akiwa ndani ya gari lake nje ya makazi yake Area D mjini Dodoma
Septemba 7, mwaka huu anazungumzia kumbukumbu ya miaka 20 akiwa amejilaza
kitandani hospitalini hapo katika mahojiano na Mwananchi.
“Mke wangu
nikuzungumziaje? Lissu anamuuliza Alicia ambaye anamjibu, “kazi kwako.”
“Mke wangu mpenzi
anaishi kiapo chake tulipooana Novemba 29, 1997, tunatimiza miaka 20
…tulipooana nilimsikia anasema ‘kwa shida na raha, nitampenda, nitafanya nini
na nini’, kwa hiyo mke wangu mpenzi anaishi katika kiapo chake,” anasema Lissu
akiwa mwenye tabasamu.
“Katika miaka
hii 20, tumepitia majaribu mengi sana, lakini hili (kupigwa risasi) ndilo kubwa
kuliko yote na nafikiri kama ni mtihani, mke wangu ameufaulu kwa daraja la juu
kabisa kwa sababu amekuwepo hapa muda wote na mara nyingine ukimsikia
anavyozungumza ana msimamo mkali kuliko mimi niliyeumizwa,” anasema mwanasheria
huyo.
“Ni mke wa
kweli, aliyekubali kuchukua majukumu ya kuwa mke, najisikia faraja na furaha ya
kipekee kwa sababu ya kuwa naye na ninamwomba tuendelee kuwa hivyo kwa miaka 20
mingine inayokuja,” anasema Lissu huku pembeni yake mkewe akitabasamu.
Anatumia muda huo
kumpa ujumbe mke wake kuwa, “najisikia mwanamme mwenye bahati sana kuwa naye,
ni mwanamke wa kipekee sana kuwa naye, tumetoka mbali sana na hii miaka 20
imekuwa mizuri sana katika maisha yangu kwa sababu ya kuwa naye.”
Alicia hakuacha
mazungumzo hayo yapite hivi hivi tu, alikuwa na mtazamo wake kuhusu safari hiyo
ya miaka 20.
“Miaka 20 ni mingi,
lakini nikifikiria ni kama juzi tu, halafu nilikuwa sitaki kumkumbusha nilitaka
kumfanyia ‘surprise,’” anasema huku Lissu akimsikiliza kwa makini na
kutabasamu.
Alicia, ambaye
kitaaluma ni wakili anasema, “lazima niwe mkweli kuna miaka mingine ilikuwa
busy anasahau hata siku…Tundu ni mume wangu, kikubwa naweza kusema ni rafiki
yangu wa karibu sana wa miaka mingi sana, nikiwa msichana mdogo, mrembo na
smati, tumekuwa tukiishi hivyo.”
“Ujumbe wangu, Tundu
siku zote aendelee kuwa Tundu tu, Tundu wa kabla ya tukio na baada ya tukio awe
ni Tundu niliyemjua siku zote,” anasema.
Tundu Lissu ambaye ni
Rais wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), ametimiza siku 84 tangu
alipopigwa risasi mjini Dodoma na kusafirishwa kwa ndege kwenda kutibiwa katika
Hospitali ya Nairobi.
Na
Ibrahim Yamola, Mwananchi



