Breaking News

GST YAWATAKA WACHIMBAJI MADINI KUACHA UCHIMBAJI WA KUBAHATISHA

Dar es salaam - Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imewataka wachimbaji wadogo na wa kati wa madini nchini kutumia wataalamu na taarifa za kisayansi za kijiojia kabla ya kuanza shughuli za uchimbaji ili kuepuka hasara zinazotokana na uchimbaji wa kubahatisha.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Kijolojia wa GST, Alex Ciprian Ruta Gorela, ambaye amesema taasisi hiyo ina wataalamu na vifaa vya kisasa vinavyoweza kusaidia kubaini maeneo yenye uwezekano wa kuwa na madini.

Amesema GST ina jukumu la kufanya tafiti za kijiojia nchini, zikiwemo uchoraji wa ramani za kijiojia (Geological Mapping), tafiti za kijiokemia (Geochemical Survey) na kijiofizikia (Geophysical Survey), pamoja na kukusanya taarifa kuhusu majanga ya asili kama matetemeko ya ardhi, mafuriko na maporomoko ya milima.

Kwa mujibu wa Gorela, katika kutafuta madini, mchimbaji anahitaji kuzingatia aina tatu za taarifa ambazo ni za kijiojia, kijiokemia na kijiofizikia, akisisitiza kuwa kutegemea taarifa za kijiofizikia pekee hakutoshi kupata matokeo yanayotarajiwa.
Amesema taarifa hizo zinapounganishwa humsaidia mchimbaji kuelewa muundo wa miamba, mwelekeo wake na maeneo yenye viashiria vya uwepo wa madini, hivyo kupunguza uwezekano wa kupoteza mitaji katika shughuli za uchimbaji.

Ameongeza kuwa GST ina timu ya wataalamu wapatao 60, wakiwemo wanajiojia na wataalamu wa fani nyingine zinazohusiana na utafiti wa miamba na madini, ambao hutoa huduma za ushauri wa kitaalamu kwa wachimbaji na wadau wa sekta ya madini.

Aidha, amesema taasisi hiyo ina vifaa vya kisasa vya kufanya tafiti za kijiofizikia, ikiwemo teknolojia ya Induced Polarization (IP Survey), vifaa vya kupima usumaku na mifumo ya upimaji wa umeme ardhini, huku ikisisitiza umuhimu wa kuwa na wataalamu wenye uwezo wa kutumia vifaa hivyo na kuchambua matokeo yake.
Amesema matumizi sahihi ya vifaa hivyo pamoja na uchambuzi wa kitaalamu wa taarifa zinazokusanywa ni muhimu katika kumwezesha mchimbaji kufanya maamuzi sahihi kabla ya kuwekeza fedha nyingi katika shughuli za uchimbaji.

Katika hatua nyingine, Gorela amewataka wachimbaji wadogo na wa kati kuacha kutegemea njia za kienyeji na imani zisizo za kisayansi katika kutafuta madini, badala yake kutumia huduma za wataalamu wa GST ili kupata taarifa zinazoweza kuwaongoza katika shughuli zao.

Amesisitiza kuwa GST ipo tayari kutoa elimu, ushauri na taarifa za kitaalamu kwa wachimbaji na wadau wote wa sekta ya madini, akiwahimiza kutembelea taasisi hiyo na kunufaika na utaalamu uliopo.