Askofu Mkuu Wa Kanisa La EAGT Atumbuliwa...Mhasibu Mkuu Naye Apitiwa

Bodi ya Wadhamini ya Kanisa la
Evangelistic Assemblies Of God Tanzania (EAGT) imemsimamisha Askofu Mkuu wa
kanisa hilo, Mchungaji Brown Mwakipesile ili kupisha uchunguzi wa tuhuma
zinazomkabili.
Wengine waliosimamishwa leo Desemba 18 ni
Katibu Mkuu, Mchungaji Leonard Mwizarubi na Mhasibu Mkuu, Mchungaji PrayGod
Mngonja.
Pamoja na mabadiliko hayo, bodi imewateua kwa
muda kushika nafasi hizo, Askofu Mkuu atakuwa ni Mchungaji Asumwisye
Mwaisabila, Katibu Mkuu atakuwa Dk Jakob Madaha na Mhasibu Mkuu atakuwa Andrea
Salu.
Kwa mujibu wa Katiba ya EAGT ya Mwaka 2011
,ibara ya 6(b)(5) kinatoa mamlaka Kwa Wajumbe wanne wa bodi hiyo kusimamisha
viongozi wakuu wa kanisa akiwamo Askofu Mkuu kabla ya Mkutano Mkuu kujadili
maazimio hayo.
"Baada ya siku 30 kuanzia leo
tutakuwa na mkutano mkuu wa Kanisa kwa ajili ya kupitisha mabadiliko hayo,
wamesimamishwa kwa kumfukuza Makamu Askofu Mkuu wakidai alitenda dhambi,
walimfukuza uchungaji na uumini pia," ni kauli ya Mwenyekiti wa bodi hiyo,
John Mfuko alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari.
Mzee Mfuko ambaye anazungumza kwa taabu
kutokana na umri wake alisema kosa la viongozi hao wa kanisa ni kumfukuza bila
kushirikisha bodi ya Wadhamini.
Mzee Mfuko aliyeongozana na wajumbe wawili kati
ya wanne wa bodi hiyo alisema licha ya mahakama kubatilisha suala la kumfukuza,
Askofu Mkuu (aliyefukuzwa) alikataa kumrejesha kanisani. Tuhuma nyingine ni
kushiriki njama za kuhujumu mali za kanisa.
Baada ya kutafutwa kwa simu yake ya mkononi,
Askofu aliyesimamishwa Mwakipesile hakupatikana kwenye simu yake ya mkononi.
Mbali na tuhuma hizo, bodi imewataka waumini wa
kanisa hilo kutotuma pesa katika akaunti za kanisa huku ikiweka wazi kushikilia
akaunti hizo kutoka mikononi mwa viongozi waliokuwa na dhamana ili kuhakiki wa
mali za kanisa.
Na Kelvin Matandiko Mwananchi



