JENGO LA TANESCO KUBOMOLEWA KWA BOMU DISEMBA 11
JENGO la Shirika la Umeme Tanzania
(Tanesco), sasa kubomolewa Desemba 11 mwaka huu huku Wakala wa Majengo Tanzania
(TBA), ikitafuta njia bora ya kubomoa jengo hilo ikiwemo matumizi ya bomu,
baruti au kwa tingatinga.
TBA ambao wamepewa zabuni ya kubomoa
jengo hilo, walishindwa kufanya hivyo Novemba 29 mwaka huu kutokana na mfumo wa
kompyuta, uliotengenezwa kwa ajili ya utoaji wa huduma za umeme kwa njia ya
luku, takwimu na samani mbalimbali zilizopo.
Akizungumzia ubomoaji huo Dar es
Salaam jana, Mkurugenzi Mtendaji wa TBA, Eliud Mwakalinga alisema kuwa
wanaendelea kutathmini njia bora ya kubomoa jengo hilo, kwa kuwa zote zina
madhara kwa watu walio karibu na jengo hilo, ikiwemo uchafuzi wa hali ya hewa.
“Tunaweza kutumia teknolojia ya bomu
kulipua jengo lote na kuisha, kutumia baruti kwa kuangalia nguzo nzito ili
kubaki na kifusi au tingatinga. Lakini tumegundua kuwa bado kuna hali ya
usalama tunatakiwa kuzingatia wakati wa ubomoaji ikiwemo vumbi litakalojitokeza,
mawe na kokoto ambazo zinaweza kuharibu vioo vya wenye magari barabarani bila
kujua,’’ alisema Mwakalinga.
Alisema kuwa wakati wa ubomoaji huo,
watazungushia wavu sehemu ya jengo lote ili vumbi na kokoto zitakazotoka katika
jengo hilo zisiweze kuleta madhara kwa watumiaji wengine wa barabara na
wananchi wanaoishi karibu na jengo hilo.
Pia alisema jengo linapojengwa,
hutumia michoro na kwamba hata kubomoa ni lazima watumie michoro ili kuona
namna inayofaa katika kubomoa. Kwamba menejimenti yote ya TBA, ambao awali
walitaka kuwapa watu wengine kazi hiyo ya ubomoaji, wamekubali kufanya hivyo
kwa kuwa ni watumishi wenzao wa serikalini.
Novemba 27, mwaka huu uongozi wa
Tanesco ulianza utekelezaji wa agizo la Rais John Magufuli, aliyeagiza majengo
ya Wizara ya Maji na Umwagiliaji na ghorofa la Tanesco, kuwekwa alama ya X kwa
ajili ya kubomolewa.
Rais Magufuli Novemba 15, mwaka huu
akitokea Chato alipokwenda kwa mapumziko baada ya ziara ya Uganda, aliagiza
Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) kuweka alama ya X katika majengo hayo
sehemu zilizo katika hifadhi ya barabara.
Tanesco ilisema baadhi ya watumishi
wa shirika hilo, walianza kuhamishiwa katika ofisi nyingine za shirika zilizopo
jijini Dar es Salaam ili kupisha shughuli za ubomoaji kufanyika kwa usalama.
Chanzo- Habarileo



