MTOTO WA KIKE WA MIAKA 7 ABAINIKA KUWA NI WA KIUME JIJINI DAR

Daktari Bingwa wa Upasuaji wa Watoto MNH, Zaitun Bokhary
NA LUCY NGOWI
MTOTO wa miaka saba
aliyelelewa kama mtoto wa kike kutokana na maumbile yake kutoeleweka vema,
baada ya vipimo vyote katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ameonekana
kuwa ni mwanamume, hivyo amefanyiwa upasuaji wa kwanza wa kushusha kokwa (mbegu
za kiume) kwenda kwenye korodani ili kumrejesha katika hali ya kawaida.
Daktari Bingwa wa
Upasuaji wa Watoto MNH, Zaitun Bokhary alisema hayo alipofanya mahojiano
maalumu na Habari Leo kuhusu kambi ya wiki moja iliyowekwa kwa ajili ya kufanya
upasuaji ambao ni mgumu, wakishirikiana na wataalamu watano kutoka Chuo Kikuu
cha Oxford nchini Marekani.
Dk Bokhary alisema
upasuaji huo ni hatua ya kwanza katika kumrejesha mtoto huyo katika hali ya
kawaida, hatua nyingine za upasuaji zitafuata, kwani atafanyiwa upasuaji kwa
hatua tatu.
Alisema kwa kuwa
mtoto huyo vipimo vimeshaonesha kuwa ni wa kiume, wametoa ushauri kwa wazazi
wake hususan baba yake kuwa karibu na mtoto huyo ili kumfanya asijisikie
vibaya, kwani awali alikuwa akijisaidia haja ndogo kama mtoto wa kike, pia
alikuwa amepewa jina la kike ikiwa ni pamoja na kuvaa nguo za kike.
“Tumemshauri baba
yake kutembea mara kwa mara na mtoto wake, pia kwenda naye katika michezo ya
kiume, ikiwa ni pamoja na kuanza kumvalisha mavazi ya kiume. “Mtoto huyu
alipoanza kuvaa nguo za kiume kwa mara ya kwanza alikuwa akijisikia aibu kwa
kuwa alishazoezwa mambo ya kike, lakini tunaendelea kutoa ushauri kwa wazazi ili
wawe karibu na mtoto wao asijisikie tofauti yoyote,” alisema daktari huyo.
Aliongeza kuwa kwa
kuwa tayari mtoto huyo alikuwa akisoma katika shule ya msingi mojawapo jijini
Dar es Salaam, hospitali hiyo inafanya utaratibu kupitia kwa daktari wake ili
kuandika barua kwa Wakala wa Usajili Ufilisi na Udhamini (Rita), atambuliwe
kama mwanamume, ikiwa ni pamoja na kuhamishwa shule aliyokuwa akisoma.
Alisema kuwa na sasa
mtoto huyo, amehamishwa nyumbani kwao anakaa na ndugu zake eneo lingine ili
aanze kuzoea mazingira mapya ya maumbile yake. Pia Dk Zaitun alielezea upasuaji
mwingine mgumu uliofanyika ni wa mtoto wa siku mbili ambaye alikuwa na tatizo katika
mfumo wa nyongo, njia ilikuwa imefungwa ilibidi apasuliwe kufungua njia ili
mfumo wa nyongo uendelee kama kawaida.
“Kwenye mfuko wa
nyongo kulikuwa kumetengeneza uvimbe nyongo isipite vizuri, hivi sasa baada ya
upasuaji anaendelea vizuri,” alisema. Daktari bingwa huyo wa upasuaji wa
watoto, alieleza upasuaji mwingine walioufanya ni kwa mtoto aliyekuwa na
saratani ya figo zote mbili, moja ilitolewa na nyingine ilikuwa haijalika
ikaondolewa sehemu ya tatizo bila kuathiri mfumo wa misuli.
Alisema upasuaji wote
huo umekwenda vizuri, hali za watoto hao zinaendelea vema. Alisema kambi ya
upasuaji huo ilikuwa Novemba 27 hadi Desemba Mosi, mwaka huu iliongozwa na
Daktari Bingwa Mshauri Mwelekezi wa Upasuaji wa Watoto, Profesa Kokila Lakhoo
kutoka Chuo Kikuu hicho cha Oxford. Alisema Dk Lakhoo amekuwa akija hospitalini
hapo kila mwaka, kusaidia ule upasuaji ambao ni mgumu, na huu ni mwaka wake wa
tano kufika nchini.



