Rais Magufuli: Wanaosema Vyuma Vimekaza Waweke Grisi La Sivyo Vitavunjika.

Rais John Magufuli amesema vyuma
vikikaza vinatakiwa kuwekwa grisi vilainike, vinginevyo vitavunjika kabisa.
Amesema hayo leo Alhamisi Desemba
14,2017 alipofungua mkutano mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT).
Rais Magufuli amesema waliokuwa
wanapata fedha kwa njia zisizo halali ndiyo wanaosema vyuma vimekaza.
“Vyuma vimekaza na bado vitavunjika
kabisa nawashauri muweke grisi,” amesema.
Msemo wa vyuma vimekaza umekuwa
maarufu katika siku za karibuni ukiwa na maana maisha yamekuwa magumu.
Rais Magufuli amesema alipoingia
madarakani alikuta changamoto nyingi zikiwemo za wafanyakazi hewa, vyeti feki
na ufisadi.
Amesema baada ya kudhibiti, watumishi
wa umma 12,000 wamepatikana na vyeti feki wakiwemo walimu 3,655 tangu
walipoanza kuhakiki.
Amesema uhakiki huo ulibaini
watumishi hewa 20,000 na kwamba, Serikali ilikuwa inapoteza fedha nyingi
kuwalipa mishahara.
“Kila kitu kilikuwa hewa hata mapenzi
inawezekana yalikuwa hewa,” amesema Rais Magufuli.
Amesema kutokana na udhibiti wa fedha
za Serikali ni lazima watu waliokuwa wanapata fedha kwa njia zisizo halali
watalalamika kuwa vyuma vimekaza.
Kuhusu madai ya walimu, amesema Sh25
bilioni wanazoidai Serikali zitalipwa baada ya uhakiki kumalizika
==>Msikilize
hapo chini==>>



