TTCL Wajilipua Sakata La AIRTEL

IKIWA imepita siku mbili tangu Rais John
Magufuli amwagize Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, kuchunguza
undani wa suala la umiliki wa kampuni ya simu ya Airtel, siri zaidi kuhusiana
na kile kilichofanyika katika ‘dili’ za mauziano zimeanza kuanikwa.
Akizungumza mjini Dodoma juzi, Rais
Magufuli alimtaka Dk. Mpango kuchunguza undani wa kampuni ya Airtel baada
ya kuwapo kwa taarifa kuwa kampuni hiyo inapaswa kuwa chini ya umiliki wa
Kampuni ya Simu (TTCL), ambayo ni ya serikali. Pia Rais Magufuli alieleza
wazi kuwa kuna ‘mchezo mchafu’ uliofanywa na baadhi ya watu katika suala hilo.
Kutokana na agizo hilo la Rais
Magufuli, jana, TTCL, kupitia kwa mwenyekiti wake wa sasa wa bodi ya
wakurugenzi, Omar Nundu, na Ofisa Mtendaji Mkuu, Waziri Kindamba, iliibuka na
kuanika undani wa mambo kadhaa kuhusiana na kampuni hiyo, mojawapo ikiwa namna
vigogo watano walivyoketi kwa siku moja na kufanya uamuzi unaoibua maswali
mengi kwa sasa kuhusiana na umiliki wa kampuni ya Airtel. Kimahesabu, siku moja
ina saa 24.
Alipoulizwa jana kuhusiana na suala
hilo linaloambatana na madai kwamba TTCL ndiyo inayoimiliki Airtel Tanzania,
Meneja Uhusiano wa kampuni hiyo, Jackoson Mbando, alisema jambo hilo hawawezi
kulizungumzia kama watendaji bali wamiliki wa hisa walio nje ya nchi ndio wenye
wajibu huo.
Akizungumza na waandishi wa habari
jijini Dar es Salaam jana, Nundu alisema chanzo cha yote kilianzia Agosti
5, 2005, wakati aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi za TTCL na Celtel wakati huo na
wajumbe watano ambao majina yao hakuwa tayari kuyataja, walipokutana siku hiyo
moja na kubariki uamuzi mzito uliofikisha jambo hilo lilipo sasa.
Nundu alisema bodi hiyo ilikuwa na
watu tisa, lakini siku hiyo moja waliketi watano kati yao na kufanya uamuzi huo
mazito huku wakiongozwa na mwenyekiti ambaye wakati huo alikuwa amekabidhiwa
asilimia moja ya hisa zilizokuwa zikimilikiwa na ‘mtu asiyejulikana’.
Nundu alisema Celnet ilianzishwa na
TTCL Mei 7, 2001 kwa mtaji wa Sh. bilioni moja na thamani ya hisa ikiwa Sh.
milioni moja.
Alibainisha kuwa TTCL ilikuwa
ikimiliki hisa moja huku thamani ya hisa ilikuwa Sh. 1,000 na mtu asiyejulikana
alikuwa akimiliki hisa moja yenye thamani pia ya Sh. 1,000, kuanza baishara kwa
jina la Celtel.
Hata hivyo, Nundu alisema hisa moja
ya mtu asiyejulikana ikashikiliwa na raia wa kigeni na kwamba baadaye, TTCL
ilitoa bilioni tano kwa ajili ya mtaji ili kampuni ianze kufanya kazi.
"Ilianzishwa kampuni inaitwa
Celnet…imeanzishwa na TTCL,…ikapewa masafa megawati 900. Ilipofika wakati wa
kufanya kazi, ikabadilishwa na kuwa Celtel, kampuni hii ilianzishwa na TTCL Mei
7, 2007 mtaji wake ukiwa Sh. bilioni moja, maana yake hisa milioni moja na kila
hisa ina thamani Sh. 1,000,” alisema Nundu.
“Lakini wanahisa wakawa wawili, TTCL
yenyewe ikachukua hisa moja, mtu asiyejulikana akachukua hisa moja, lakini
akaishika raia wa kigeni. Kwa maana hiyo, kampuni ikaanzishwa kwa fedha Sh.
2,000," alisema Nundu.
Aidha, Nundu alisema TTCL ilitoa pia
fedha zaidi ya Sh. bilioni 82 kwa ajili ya biashara huku cha kushangaza, mtu
asiyejulikana akiwa hajatoa kitu chochote.
"Kama si TTCL kutoa Sh. bilioni
tano, hakuna ambacho kingefanyika. Hakukuwa na uhitaji wa
mwekezaji…. isitoshe TTCL iliweka Sh. bilioni 82 na ushee kuikopesha
Celtel…sasa hapo unaona ni kampuni ya TTCL," alisema Nundu.
Alisema baadaye, raia wa kigeni
aliyekuwa akishikilia hisa moja ya mtu asiyejulikana aliikabidhi kwa Mtanzania
ambaye alikuwa miongoni mwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya TTCL na pia
Celtel.
“Siku ya kikao hicho, mwenyekiti wa
bodi (ambaye ndiye aliyekabidhiwa hisa hiyo moja ya mtu asiyejulikana) na
wajumbe wengine watano walifanya maamuzi (uamuzi) magumu (mgumu) ya kuirudisha
hisa hiyo moja na kuikabidhi TTCL, hivyo TTCL ikawa inamiliki Celtel kwa hisa
zote kwa asilimia 100,” alisema.
Akieleza zaidi kuhusiana na ‘mchezo’
uliofanyika, Nundu alisema thamani ya hisa asilimia 100 za TTCL ilikuwa Sh.
bilioni moja, lakini wakakubaliana siku hiyo kuongeza thamani ya hisa hizo hadi
kufikia Sh. bilioni 50 katika kampuni ya Celtel.
Alisema mpaka Mei 7, 2001, hisa
999,998 zisizo na mtu ilipewa TTCL kwa sababu ilishaweka Sh. bilioni tano,
hivyo kuwa na jumla ya hisa 999,999 huku mtu asiyejulikana akiwa bado anamiliki
hisa moja.
Nundu alisema ilipofika Novemba 27,
2001, raia wa kigeni aliyeshikilia hisa ya mtu asiyejulikana alimpa mtu
mwingine ashikilie ambaye ni Mtanzania, na mtu huyo aliyepewa ashikilie ndiye
aliyekuwa mwenyeki wa bodi ya TTCL na Celtel.
Nundu aliongeza kuwa baada ya hapo,
zilichukuliwa Sh. bilioni 40 za TTCL na kuwekwa katika mfuko wa Celtel kama
mtaji wake, hivyo kuifanya kumilikiwa kwa asilimia 100 kwa mtaji wa Sh. bilioni
41, huku Sh. bilioni tisa zikiwa hazina mmiliki.
“Siku hiyo hiyo moja, baada ya muda
TTCL ikanyang’anywa hisa zake zote na hapo ndipo tunapojiuliza uhalali wa
Celtel,” alisema Nundu.
Nundu alisema kama hiyo
haitoshi, hisa hizo zilianza kugawanywa kwa watu ambao hawapo katika mlolongo
wa Celtel kutokana na ukweli kuwa wakati huo, waliokuwa wakitambulika ni
wawili tu, yaani TTCL na ‘mtu asiyejulikana’.
Aidha, alisema ilikubaliwa kuwa
serikali ipewe asilimia 65 na ‘mtu asiyejulikana’ apewe asimilia 35.Alisema kwa
hesabu za kawaida, haikupaswa watu wengine kugaiwa hisa kwa sababu hawakuwa na
hisa tangu awali lakini wakapewa hisa zote.
Alisema kama haitoshi, siku hiyo hiyo
ya kikao cha bodi yenye watu watano, serikali ikapewa hisa milioni 26.650,
ikiwa ni uwiano wa asilimia 65 ya umiliki na mwingine (mtu asiyejulikana)
alipewa hisa milioni 14.350, sawa na asilimia 35.
Baada ya hapo, alisema serikali
ilichukua tena hisa milioni 10 zingine na kumpa mwekezaji, hivyo kumfanya
afikishe milioni 24.350 na kuifanya serikali kubakiwa na hisa milioni 16.650.
Alisema uwiano huo ndio unaoendelea
hadi leo na kwamba umiliki wa Celtel upo mikononi mwa Airtel ‘kimagumashi’
(kijanjaujanja).
Kadhalika, Nundu alisema jambo la
kushangaza ni kwamba ilipofika Juni 23, mwaka jana, Airtel ilitangaza kujitoa
kwenye umiliki wa TTCL ambao walikuwa wamiliki na wameshajitoa.
Nundu alisema baada ya kufanyika ‘mchezo’
huo, TTCL ilikopeshwa dola za Marekani milioni 28 na kuwekewa riba ya
asilimia 18 na kusababisha deni kukua hadi kufikia Sh. bilioni 76.6.
“Mimi na wenzangu baada ya kuja TTCL,
ndiyo tukaanza kuchimba chimba ili kujua mbivu na mbichi kwa sababu kuna mambo
mazito zaidi,” alisema.
Bosi TTCL Ajilipua
Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTCL, Waziri
Kindamba, alisema wanachotaka kutoka kwa Airtel ni kampuni yao.
Alisema wanaamini na kutarajia kuwa
watarejeshewa kampuni yao bila kukwaruzana na wamikili wa kampuni ya Airtel na
kwamba wamejipanga kwa ushahidi wa asilimia 100.
“Tumeamua kujitoa sadaka za nafsi na
miili yetu kwa ajili ya kutetea wanyonge katika vita hii kubwa ya uchumi
inayoongozwa na Rais Magufuli,” alisema Kindamba.
Pia alisema wanatarajia kufanya
biashara ya huduma za simu kwa gharama nafuu zaidi watakaporejeshewa kampuni
yao na pia kuiwezesha kulipa kodi zaidi serikalini.



