TUNDU LISSU ATUMA SALAMU WIKI YA MSAADA WA SHERIA....AWATAKA WATANZANIA WASICHOKE KUMUOMBEA

Rais wa Chama cha
Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Tundu Lissu ametumia maadhimisho ya wiki ya
msaada wa sheria kuwaomba wananchi kumwombea apone na kurudi nchini aendelee
kutoa mchango wake katika taaluma ya sheria.
Lissu tangu
Septemba 7 amelazwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya anakopatiwa
matibabu baada ya kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi akiwa katika makazi
yake Area D mjini Dodoma.
Akizungumza leo
Jumatatu Desemba 4,2017 katika ufunguzi wa wiki ya msaada wa sheria, mwakilishi
wa TLS, John Seka amesema Lissu anawasalimia wananchi.
“Rais wa TLS, Tundu
Lissu anawasalimia sana, anaendelea kupata nafuu ila anawaomba Watanzania
waendelee kumwombea ili apone haraka,” amesema Seka.
Amesema Lissu ambaye
pia ni mbunge wa Singida Mashariki (Chadema) ana hamu ya kurudi nyumbani
aendelee kutoa mchango wake wa kisheria kwa wananchi.
Kuanzia leo hadi
Desemba 8,2017 wananchi wanapata fursa ya kupata msaada wa kisheria katika
migogoro inayowakabili.
Seka ametoa wito
kwa wananchi kufika katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam na
mikoani kupata huduma ya msaada wa kisheria.
Amesema baada ya
wiki hiyo kumalizika, wananchi watatakiwa kufika ofisi za TLS kupata msaada wa
kisheria kwa kuwa hilo ni moja ya majukumu ya chama hicho.



