Mbunge Aliyesimamia Kiapo Cha Raila Odinga Akamatwa

Mbunge wa Ruaraka Tom J Kajwang’, ambaye
alisimamia “kuapishwa” kwa kiongozi wa muungano wa Nasa Raila Odinga kwenye
viwanja vya Uhuru Park Jumanne amekamatwa.
Mbunge huyo amekamatwa leo Jumatano
mchana na maofisa wa polisi ambao hawakuwa wamevalia sare nje ya Mahakama ya
Milimani jijini Nairobi.
Alikamatwa muda mfupi baada ya
kuhudhuria katika Mahakama Kuu mbele ya Jaji George Odunga kusikiliza uamuzi wa
kesi aliyowawakilisha wabunge wanaopinga kukatwa mishahara yao na posho.
Kajwang’ na mwanasheria mwingine
Miguna Miguna, ndio walikuwa wasimamizi wakuu wa matukio ya kwenye viwanja vya
Uhuru Park yaliyomalizikia kwa “kuapishwa” Odinga kama ‘rais wa watu’.
Wakati wa sherehe za kiapo Kajwang’
alikuwa amevaa vazi na wigi na alishangiliwa sana na wafuasi wa Nasa.
Odinga alikula “kiapo” huku Kajwang’
akiwa amesimama nyuma yake japokuwa wajibu wake katika tukio hilo bado
haujafahamika.



