Aliyekamatwa Uwanja Wa JNIA Na Dawa Za Kulevya, Aendelea Kutoa Pipi Tumboni

Raia wa Nigeria, Christian Ugbechi
(26) aliyekamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) baada
ya kukutwa na pipi 59 za dawa za kulevya aina ya Cocaine, jana Januari 31, 2018
ametoa pipi nyingine 23.
Ugbechi alikamatwa Januari 29, 2018
akiwa anasafirisha dawa hizo za kulevya kwenda nchini Ufaransa, huku akiwa
ameficha pipi 59, kati ya hizo 56 alizificha kwenye soksi iliyokuwa katika begi
lake la mgongoni, tatu alizitoa kwa njia ya haja kubwa.
Baada ya kudakwa, alikiri kuwa na
pipi nyingine tumboni lakini leo Kamanda wa Polisi wa Viwanja vya Ndege,
Matanga Mbushi ameliambia Mwananchi kuwa mtuhumiwa huyo ametoa pipi nyingine
23, kufanya idadi yake kuwa pipi 82.
“Kwa maelezo ya mtuhumiwa anadai
ameshamaliza kuzitoa pipi zote tumboni lakini tunaendelea kumuweka chingi ya
uangalizi maalum,” amesema Mbushi na kuongeza,
“Bado tunamfuatilia kwa maana ya kila
anapokwenda haja kubwa, lengo ni kujipa uhakika kama kweli amemaliza pipi
hizo.”
Na Pamela Chilongola,Mwananchi



