Naibu Meya Manispaa Ya Iringa Ajiuzulu

Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa,
Dady Igogo ameandika barua ya kujiuzulu wadhifa wake wa Naibu meya .
Kwamujibu wa barua yake ya Februari
13 aliyoiwasilisha kwa Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo, Alex Kimbe, Igogo amedai
ameamua kujiuzulu wadhifa huo na kwamba atabakia na wadhifa wake wa udiwani.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya
Manispaa ya Iringa, Omary Mkangama amethibitisha kupokea nakala ya barua ya
kujiuzulu kwa naibu meya na kwamba hajatoa sababu za kujiuzulu wadhifa huo.
"Nikweli taarifa hizo ni za
kweli, nimepata nakala ya Naibu Meya kujiuzulu wadhifa huo na kubaki diwani
kata ya Gangilonga lakini hajatoa sababu za uamuzi wake" amesema Mkangama.
Jitihada za kutafuta Mstahiki Meya wa
Manispaa hiyo, Alex Kimbe kuzunguzia taarifa hizo hazikuzaa matunda baada ya
simu yake kuita bila kupokelewa.
Pia Igogo naye simu yake imeita bila
kupokelewa.
Igogo amejiuzulu nafasi hiyo ya Naibu
Meya wakati ambapo waliokuwa madiwani wa Halmashauri hiyo wapatao Tisa wakiwa
wamejiuzulu nyazifa zao na kujiunga na CCM.
Kati ya Madiwani waliojiuzulu nyazifa
zao ni sita kutoka katika kata na watatu viti maalum.
Kata ambazo waliojiuzulu ni Kata ya
Kitwiru ambayo katika Uchaguzi mdogo uliofanyika Novemba 26 aliyekuwa diwani wa
kata hiyo Baraka Kimata alifanikiwa kutetea kitu chake safari hii akipeperusha
bendera ya CCM.
Kata nyingine ni Kihesa ambao
Uchaguzi uliofanyika Januari 13 ambao Juli Sawani CCM ilipita bila kupingwa
baada ya vyama Vya upinzani kususia Uchaguzi.
Kata nyingine ambazo ziko wazo hadi
sasa ni Kwakilosa, iliyokuwa ikishikiliwa na Joseph Ryata aliyekuwa Naibu Meya,
kata ya Mkwawa iliyokuwa ikiongozwa na Osca Kafuka, Mwangata Angelus Mbogo na
Ruaha Gabriel Ndes.
Na Geofrey Nyang'oro- Mwananchi



