Waziri KIGWANGALLA Amjibu MANGE KIMAMBI

Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt.
Hamisi Kigwangalla amefunguka na kujibu hoja ambayo Mwanaharakati wa mambo ya
siasa mtandaoni, Mange aliibua kwenye mtandao wake Instagram kudai Waziri huyo
ameshiriki kuwaingiza chaka Watanzania ili watapeliwe pesa
Waziri Kigwangalla akijibu hoja hiyo
amesema kwamba yeye alialikwa kama mgeni wa heshima na kuwa alikuwa hawatambui
watu hao binafsi na wala biashara yao alikuwa haitambui na alipoitwa kuzindua
tawi lao hapa nchini alishindwa kuwakatalia ila hana maslahi binafsi katika
kampuni hiyo.
"Nimeona nitoe ufafanuzi kwenye
hili jambo. Maana kila mjadala juu ya hii kampuni ya ..... unapoibuka, jina
langu linakuja, na mara nyingine picha yangu inawekwa. Ukweli ni kwamba,
nilialikwa kwenye shughuli ya uzinduzi wake kama mgeni wa heshima; mgeni rasmi
alikuwa ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa wakati
huo, Dr. Adelhelm Meru.
"Niliamini kwa heshima ya
kuzinduliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji,
ambao ndiyo wenye dhamana ya usajili wa biashara zote nchini, ni lazima ni watu
halali na bado ninaamini kama kuna shida mamlaka husika zitachunguza na
kuchukua hatua stahiki na kama hakuna shida basi ni vema mamlaka husika zikatoa
mwongozo utakaowaondoa hofu wananchi wenzetu wenye ‘interest’ ya kushiriki
kwenye biashara hii.
"Baada ya kufika eneo la tukio,
kiitifaki ikaonekana nami lazima nishiriki zoezi, nikashindwa kukataa. Nadhani
inafahamika kwamba nimekuwa mstari wa mbele kuunga mkono kwa vitendo jitihada
nyingi mbalimbali za wajasiriamali vijana ambao wameamua kutoka
#NjeYaBox.
"Hata hawa nilishindwa
kuwakatalia. Ukweli ni kuwa, siwajui wao binafsi ‘at personal’ level na wala
biashara yao, umiliki wake na muundo wake siujui zaidi ya kuelewa kwa juu juu
kuwa ni ‘network marketing’.
"Ifahamike hapa kuwa sina
maslahi yoyote yale kwenye biashara hii na wala sikushiriki uzinduzi wake kwa
malengo ya kutoa ushawishi ili watu wajiunge, na natoa rai kwamba wanaotaka
kujiunga ama kuacha kujiunga wasitumie picha za ushiriki wangu siku ya
uzinduzi, kwa namna yoyote ile, kujenga uhalali wa aina yoyote ile, bali
watumie vipimo vyao vingine kufanya uamuzi na siyo picha zangu" alisema
Kigwangalla
Mbali na hilo Waziri Kigwangalla
aliwaonya watu mbalimbali na Taasisi ambazo zimekuwa zikitumia picha yake hiyo
kwa lengo la kuhamasisha watu kushiriki katika biashara hiyo na kusema
hatahusika na matokeo yoyote yale na kuwa akibaini kuna mtu au Taasisi inafanya
hivyo atachukua hatua za kisheria.
"Sintohusika na matokeo yoyote
yale, chanya ama hasi, ya ushiriki wa mtu yeyote yule ama taasisi yoyote ile,
kwenye shughuli za kampuni hii.
"Naomba pia izingatiwe kwamba,
jina langu ama picha yangu haijaruhusiwa kutumika kama bango la matangazo ya
biashara ya mtu au taasisi yoyote ile, na hivyo kufanya hivyo ni kosa kisheria
na ikibainika nitachukua hatua kali za kisheria" alisisitiza



