Breaking News

Dkt. NDUGULILE: Marufuku Waganga Wa Tiba Asili Kuweka Matangazo Kinyume Na Taratibu Za Wizara Ya Afya.

SERIKALI imetoa onyo kwa Waganga wa kienyeji, tiba asili na tiba mbadala kutoa matangazo kwenye mabango kinyume na taratibu za Msajili wa Tiba asili na Tiba mbadala kutoka Wizara ya Afya. 

Hayo yamesemwa na Naibu  Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Dkt. Faustine Ndugulile wakati alipotoa hotuba yake kuhusu Tiba asili na tiba Mbadalaa leo jijini Dar es salaam. 

"Marufuku kwa waganga wa kienyeji, waganga wa tiba asili na tiba mbadala kutoa matangazo yanayosema wanganga wanaponya magonjwa ya aina gani kwenye jamii bila ya kupata kibali kutoka Baraza la Tiba asili na Tiba Mbadala kutoka Wizara ya Afya" alisema Dkt. Ndugulile.

Aidha Dkt. Ndugulile amemuagiza Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Mpoki Ulisubisya kuwaagiza Mamlaka ya Mawasiliano Nchini TCRA kuwachukulia hatua vyombo vyote vya habari vinavyorusha matangazo ya waganga wa kienyeji, tiba asili na tiba mbadala kinyume cha taratibu za Serikali. 

Aidha Dkt. Ndugulile amesema kuwa marufuku kwa waganga wa tiba asili na tiba mbadala kuingiza mashine ikiwemo phanta  wanazoziita zinatibu magonjwa fulani kwani hazijathibitishwa  na Serikali kupitia Wizara ya Afya kama zina ubora wa kutibu magonjwa hayo kweli. 

Mbali na hayo Dkt.  Ndugulile amesema kuwa waganga wote wa asili na tiba mbadala kwenda kujisajili na kusajili dawa zao ili zitambulike kisheria na kuepusha madhara kwa watumiaji. 

Kwa upande wake Msajili wa Baraza la Tiba asili na Tiba Mbadala  Ruth Suza kuwa amesema kuwa  mpaka sasa dawa aina tano ndizo zilizothibitishwa na kusajiliwa hapa nchini kwa ubora na matumizi ya  wananchi.