DSE Yafafanua Kuhusu Kuporomoka Kwa Mauzo Ya Hisa

Kufuatia baadhi ya watu katika mitandao ya
kijamii kuhusisha upunguaji wa mauzo ya Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) na
hali ya uchumi, Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko hilo Bw. Moremi Marwa ametoa
ufafanuzi wa muenendo wa soko hilo.
Amesema kupungua
huko ni hali ya kawaida katika soko kunakotokana na wawekezaji kupendelea
kubadili uwekezaji kutoka kwenye hisa kwenda kwenye hati fungani, na kwamba
hali hiyo ikitokea mauzo ya hisa hushuka wakati ya hati fungani yakipanda.
Huku akirejea
takwimu zinazoonyesha mwenendo wa soko katika kipindi cha robo mwaka wa 2017 na
2018, amesema kuanzia Januari hadi Machi 10 mwaka huu kulikuwa na miamala ya
mauzo ya hisa zenye thamani ya jumla ya Sh. bilioni 72 na mauzo ya hati
fungani-Bonds yalikuwa na thamani ya bilioni 287 kwa bei ya kuuzia.
Ukilinganisha na
kipindi cha robo mwaka cha 2017 ambapo kulikuwa na miamala yenye thamani ya sh.
75 na thamani ya bonds ilikuwa bilioni 229, na kwamba mwaka huu mauzo ya bonds
yalipanda kwa bilioni 58 hali iliyopelekea kushuka kwa mauzo ya hisa.
“Tunaweza kusema
mwenendo ni kuwa wawekezaji wana hama kati ya hisa na hati fungani, hii ni
hulka ya kawaida ya soko na wawekezaji, pia viashiria vingine kama market capitalization
na indices karibu zote zinapanda ukilinganisha na mwaka uliopia,” amefafanua.
Ameongeza kuwa,
“Mlinganisho wa kila wiki hasa ukizingatia kwa muktadha wa maendeleo na uchanga
wa soko letu na mauzo kwa vipindi vya muda mfupi kama vile siku au wiki
haielezi upana na uhalisia wa mwenendo wa soko.”



