LISSU Kurejea Nchini Baada Ya Kufanyiwa Upasuaji Wa Mguu?

Alute Mughwai,
kaka wa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu amesema ndugu yake
atakaa kwa wiki mbili katika hospitali ya Leuven Gasthuisberg ya nchini
Ubelgiji baada ya kufanyiwa upasuaji wa mguu wake wa kulia.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo Machi 15, 2018 Mughwai amesema kutokana na operesheni
hiyo, Lissu ambaye alikuwa akipatiwa matibabu hospitali na kurejea kwenye
makazi yake, sasa atakaa hospitali kati ya siku saba hadi 10.
Amesema upasuaji
katika mguu huo, ambao awali ulionekana kutounga vizuri, ulikwenda vizuri na
madaktari wa hospitali hiyo wamemtaka alazwe ili kupata matibabu zaidi.
Wakili Mughwai
ambaye ndiye msemaji wa familia ya Lissu, amesema baada ya siku 10, Madaktari
watatoa taarifa juu ya maendeleo ya afya yake na mazoezi ya viungo ambayo
alikuwa anaendelea nayo.
"Kutokana na
maelekezo ya madaktari kwa sasa, hatuwezi kusema Lissu atarudi lini nchini,
kwani upasuaji wa jana umesababisha alazwe tena hospitali"alisema.
Amewaomba Watanzania
na watu wengine, kuendelea kumuombea Lissu ili apone haraka na arejee nchini.
Akizungumzia
matibabu ya Lissu, amesema wanaomba watanzania na wasamaria wema, kuendelea
kumchangia Lissu kupitia akaunti iliyotolewa na Chadema.
“Bado tunafanya
mazungumzo kujua kama itawezekana awe na akauti nyingine Ubelgiji ili kusaidia
matibabu kwani hadi sasa anatibiwa kwa misaada wa watanzania na watu wengine
kutoka nje ya Tanzania,” amesema
Mbunge wa Singida
Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ambaye ni rais wa Chama cha Wanasheria
Tanganyika (TLS) jana Machi 14, 2018 alifanyiwa upasuaji wa mguu wa kulia kama
alivyoshauriwa na madaktari wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Leuven, Gasthuisberg
nchini Ubelgiji.
Lissu amesema
operesheni hiyo iliyochukua saa mbili ilifanywa na timu ya madaktari bingwa
chini ya uongozi wa Profesa Willem-Jan Mertsemakers.
“Operesheni
ilienda vizuri na kwa sasa naendelea na dawa na mapumziko hospitalini kwa muda
wa angalau wiki tatu zinazokuja,” amesema Lissu.
“Wameniwekea chuma
cha kuimarisha mfupa wote wa paja la kulia. Pia wamechukua vipimo ili kuangalia
kama hakuna tatizo la bacteria kabla hawajafunga kabisa sehemu ya kwenye goti
ambayo haijaunga hadi sasa.”
Mke wa Lissu,
Alicia amesema anamshukuru Mungu kwamba upasuaji huo umekwenda vyema.



