LOWASSA : Mkapa Amegusia Ajenda Yangu Tangu Ccm....Chadema

Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa
amemueleza Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kwamba kauli yake
aliyoitoa juzi akitaka kuwepo kwa mjadala wa kitaifa kujadili hali ya elimu
nchini ilikuwa ajenda yake tangu alipokuwa CCM.
Lowassa ametoa kauli hiyo leo Machi
19, 2018 katika taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyotolewa na msemaji wake,
Aboubakar Liongo.
Katika taarifa hiyo, Lowassa ambaye
alijiunga Chadema mwaka 2015 baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa kura
za maoni ndani ya CCM kusaka mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu
uliofanyika Oktoba 25, 2015, amesema suala la elimu pia lipo katika ilani ya
uchaguzi ya Chadema.
Juzi jioni katika hafla ya kumuaga
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Profesa Idris Kikula, Mkapa
amesema kuna janga katika elimu nchini na kushauri kuitishwa kwa mdahalo wa
wazi utakaoshirikisha makundi yote ya jamii kwa ajili ya kujadili suala hilo.
Katika taarifa yake hiyo, Lowassa
amesema amesoma na kusikia taarifa ya Mkapa akitaka kuwepo kwa mdahalo wa
kitaifa kuhusu kushuka kwa elimu nchini.
“Nimefurahi kuwa Mkapa ameliibua
suala hili kwani hiyo ilikuwa ni ajenda yangu ya kwanza tangu nikiwa ndani ya
CCM na nje ya CCM. Pia Ilani ya uchaguzi ya Chadema, elimu ndio ilikuwa ajenda
kuu na tulisema tutaita mjadala wa kitaifa kuhusu elimu na kuangalia wapi
tumekwama na nini kifanyike,” amesema Lowassa.
Lowassa amedai ajenda hiyo sio ya CCM
na hawataweza kuisimamia kwa sababu wanataka kuendelea kutawala,ila hawataki
Taifa lililoelimika vizuri na linaloweza kuhoji.
Na Bakari Kiango, Mwananchi



