Maaskofu Wawili Wawapinga Wenzao Wa Kkkt Na Katoliki
Maaskofu wawili wamepinga matamko
yaliyotolewa hivi karibuni na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT)
na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Askofu wa Kanisa la Anglikana
Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), Dk Dickson Chilongani na Makamu wa Askofu
Mkuu wa Kanisa la Kibaptisti Tanzania, Michael Nhonya, wamesema viongozi wa
dini wanatakiwa kubaki kuwa walezi, washauri, wakemeaji, wenye kuonya na
kuelimisha jamii ili Watanzania waendelee kuishi kwa umoja na amani na kuwataka
wajipime wanapelekaje ujumbe wao wa kinabii kwa viongozi wao.
Askofu wa Kanisa la Anglikana
Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), Dk Dickson Chilongani amepingana na matamko
yaliyotolewa na viongozi wa dini kuhusu mwenendo wa Serikali iliyoko
madarakani.
Akihubiri katika ibada ya Pasaka
iliyofanyika katika Kanisa la Roho Mtakatifu mjini Dodoma, Askofu Chilongani
alisema, “Hivi karibuni kumekuwa na matamko yanayotolewa na baadhi ya viongozi
wa madhehebu ... Sipo hapa kumuhukumu mtu kwa sababu Yesu Kristu anasema
msihukumu msije mkahukumiwa.”
Alisema si kusudi lake kutetea
Serikali iliyoko madarakani lakini kwa habari waliyoisoma kuna tofauti kubwa
kati ya mfalme Farao na Serikali nchini.
Askofu Chilongani alikosoa njia ya
kufikisha ujumbe kwa Serikali akisema katika Biblia, Musa alikabiliana na Farao
ana kwa ana akimtaka awaruhusu wana wa Israel waende Kanani kumuabudu Mungu au
awe tayari kupokea mapigo ya Mungu.
“Ikiwa kweli Serikali iliyopo
madarakani ina kasoro, kuna njia sahihi ya kupitia ili kuitaka ibadilike. Je,
sisi viongozi wa dini tumeshindwa kwenda Ikulu au mahali pengine popote
kukutana na viongozi wetu ambao tena ni waumini wetu hadi tukimbilie kutoa
matamko. Je, huko si kuchochea vurugu.” alihoji.
Alisema kwa miaka yote viongozi wa
dini huungana kutoa matamko ya pamoja panapokuwa na ulazima, hivyo kuhoji
inakuaje leo kila dhehebu liwe na tamko lake.
Askofu Chilongani alisema wakati huu
wa Pasaka viongozi wa dini wajipime wamepelekaje ujumbe wao wa kinabii kwa
viongozi wao.
Makamu wa Askofu Mkuu wa Kanisa la
Kibaptisti Tanzania, Michael Nhonya akihubiri katika ibada ya Pasaka mjini
Dodoma jana, aliwaonya viongozi wa dini kutokuwa vyanzo vya kusababisha vurugu.
Alisema viongozi wa dini wanatakiwa
kubaki kuwa walezi, washauri, wakemeaji, wenye kuonya na kuelimisha jamii ili
Watanzania waendelee kuishi kwa umoja na amani.
Pia aliwatahadharisha Watanzania
kutojiingiza kwenye siasa zinazoashiria uchochezi unaoweza kuleta chuki na
vurugu kwa kuwa zinaweza kusababisha watu wakagawanyika.
“Viongozi wa vyama vya siasa wakae
meza mmoja kwa ajili ya maridhiano badala ya kunyoosheana vidole ambavyo
vimekuwa vikisababisha chuki miongoni mwa Watanzania,” alisema.
Alisema wakikaa pamoja wataweza
kuondoa tofauti walizonazo.
Msimamo wa Askofu Shoo
Jana, akitoa salamu za Pasaka katika
Usharika wa Moshi Mjini, Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Frederick Shoo alisema hawataogopa kuitwa majina
yoyote na watu wanaotaka kupotosha ujumbe uliopo katika waraka uliotolewa na
maaskofu.
Alisema kuna kitu ambacho Mungu
anataka kuwaambia Watanzania kupitia waraka uliotolewa na maaskofu 27 wa kanisa
hilo pamoja na ule uliotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC).
Alitoa kauli hiyo ikiwa ni siku moja
baada ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo
kumwandikia barua kiongozi huyo wa KKKT akimueleza kuwa ni muhimu kwa kanisa
kupima kwa umakini mkubwa uzito wa kila neno kabla ya kutoa kauli kwa umma.
Profesa Kitila katika barua yake
yenye kurasa sita na maneno 2,800, alisema anatoa maoni yake binafsi akiwa ni
muumini wa kanisa hilo kuhusu maudhui ya waraka wa maaskofu hao 27 wa kanisa
hilo uliotolewa Machi 24.
Dk Shoo bila kutaja majina, alisema
baada ya waraka wa TEC na ule wa KKKT kutolewa, kuna watu wachache wameibuka
wakipotosha na kupinga, huku wengine wakidai maaskofu wanasema kwa sababu
sadaka zimepungua.
Februari 11, TEC ilitoa ujumbe wa
Kwaresima wa mwaka 2018 ndani yake maaskofu wakitoa msimamo kuhusu masuala ya
kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Tangu kutolewa kwa waraka wa maaskofu
wa TEC na ule wa KKKT, kumekuwa na mijadala kadhaa nchini kuhusu
walichozungumza viongozi hao wa dini.
Dk Shoo alisema anasikitika kwamba
wanaposema jambo la ukweli linalohusu maisha ya Watanzania wote, watu wachache
wanaibuka kupotosha.
“Katika waraka tuliotoa kuna watu
wachache, nasema wajinga, wanasema maaskofu sasa wanasema kwa sababu sadaka
zimepungua kanisani, sisi sadaka hazijapungua na Wakristo wameendelea kujitoa
sana, hivyo hatujapungukiwa na kitu,” alisema Dk Shoo.
Alisema wataendelea kusema kweli na
wanaotaka kuharibu ukweli huo waendelee kuharibu kwa kuwa Watanzania walio
wengi, wenye hekima wanaelewa maneno yaliyozungumzwa si ya kujibiwa
harakaharaka tu, bali ni ya kututafakarisha.
Alisema wataitwa majina mengi lakini
wanajua ni jitihada za upotoshaji kwa ukweli uliopo katika waraka. Alisema si
jambo la kawaida kwa maaskofu wa makanisa makubwa mawili nchini kukaa kwa
nyakati tofauti na kutoa waraka wenye ujumbe mmoja.
“Hatukukaa na kupanga tutoe waraka
lakini Baraza la Maaskofu Katoliki walikaa na kuja na waraka nasi KKKT tukakaa
tukaja na waraka ukilinganisha ujumbe ni uleule. Kuna kitu Mungu anataka
kutuambia kama Watanzania kupitia ujumbe ule,” alisema.
Dk Shoo alisema, “Mungu awaguse hao
ambao wanatumia nguvu nyingi kutaka kupotosha, wanatumia nguvu nyingi kupaka
tope ili waweze kurejea katika yale yaliyotajwa pale wakayatafakari na kama
kuna hatua za kuchukua wakachukue.”
Akitoa ujumbe wa Pasaka, Dk Shoo
aliwataka Watanzania kukataa nguvu zote zinazopinga uhuru, uhai, kuharibu
maisha ya watu na kutia hofu kwa kuwa ufufuko wa Yesu umetoa mwanga na kuwaweka
watu huru.
Alisema vitisho vya watawala vinaweza
kuwafanya watoto wa Mungu wakatamani au kuendelea kukaa katika giza kutokana na
hofu.
Aliwatia moyo walioelemewa na mizigo
kutokana na ukandamizaji uliopo katika mifumo mbalimbali akisema Yesu amefufuka
ili watu wote wawe huru.
Katika mahubiri yake, Askofu wa
Kanisa Anglikana Dayosisi ya Kagera, Darlington Bendankheha aliwataka watendaji
wa Serikali kutowanyamazisha viongozi wa dini, bali wakubali kukosolewa
panapoonekana kukiukwa utaratibu wa kisheria, kiimani au kiserikali.



