Katibu Mwenezi CCM Apigwa Risasi na 'Watu Wasiojulikana'

Aliyewahi kuwa Katibu Mwenezi, CCM
Wilaya ya Sumbawanga Mkoani Rukwa Ndg. Benedict Chapewa ameuawa kwa kupigwa
risasi na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa
Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando amesema kuwa Bw. Chapewa alivamiwa na kundi
la watu wasiojulikana wakati akiwa anakunywa pombe katika moja ya baa
anayomiliki kijijini hapo.
Kamanda Kyando amesema kuwa Chapewa
ambaye ni Mtendaji wa Kata ya Mwandui iliyopo mwambao wa bonde la ziwa Rukwa
alimiminiwa risasi na watu hao kwa kutumia bunduki aina ya gobore kisha kumkata
kata na mapanga sehemu mbalimbali za mwili wake.
Hata hivyo amesema kwamba baada ya
wauaji kutekeleza adhima yao waliondoka kuelekea kusikojulikana na hawakuchukua
kitu chochote kutoka kwa marehemu wala katika baa hiyo.
Kamanda Kyando amesema uchunguzi wa
kina kuhusu tukio hilo unaendelea kufanyika na watuhumiwa wanasakwa popote
walipo ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.



