Waziri NDALICHAKO Atoa Maagizo NACTE, TCU

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako.
Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ameagiza Tume ya Vyuo Vikuu
Tanzania (TCU), Baraza la Vyuo vya Ufundi (Nacte) kufanya mapitio upya ya
nyenzo wanazotumia kukagulia ubora wa vyuo.
Profesa Ndalichako
amesema vikibainika havina ubora wavifungie mara moja hata kama ni vya
Serikali.
Akijibu hoja za
wabunge leo Mei 2, 2018 bungeni mjini Dodoma walipojadili bajeti ya wizara yake
ya mwaka 2018/19 amesema kuna baadhi ya wabunge wamelalamikia kuhusu wahitimu
wa vyuo kushindwa kuandika wasifu.
“Nacte na TCU
wamekuwa wakifungia vyuo vingi sana, lakini tatizo badi lipo, kwa hiyo
naviagiza vyombo vya udhibiti wa elimu kufanyia mapitio upya ya nyenzo za
ukaguzi ikiwemo sifa za walimu, mitihani inayotolewa na usahihishaji wao,”
amesema Profesa Ndalichako.
“Iwapo watabaini
havikukidhi ubora wavifungie bila kuogopa mtu yeyote hata kama vikiwa vya
Serikali, vifungiwe.” ameongeza
Waziri huyo
amewaagiza maofisa elimu nchini kusimamia kwa karibu ubora wa elimu katika
shule zilizopo katika maeneo yao huku akidai kitendo cha kumfukuza mwalimu mkuu
na kumuacha ofisa elimu wa eneo husika ni uonevu kwa sababu wao ndiyo wanapaswa
kusimamia ubora wa elimu.
“Utakuta ofisa
elimu ana shule tano tu lakini anashindwa kuzisimamia na Serikali haitakubali
kuwa na viongozi mizigo,” amesisitiza Waziri huyo.



