WAMBURA Nalipwa Mil.7… Watia Saini TFF Walighushiwa

Dar es salaam:
Ofisa Mtendaji Mkuu
wa Bodi ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface
Wambura (49) ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa anapokea mshahara
wa Shilingi Milioni 7 kwa mwezi.
Wambura ameyaeleza
hayo wakati akitoa ushahidi katika kesi ya utakatishaji fedha inayomkabili,
aiyekuwa rais wa TFF Jamal Malinzi na wenzake mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,
Wilbard Mashauri.
Akiongozwa na
wakili wa utetezi, Richard Rweyongeza kutoa ushahidi wake, Wambura amebainisha
kuwa aliwahi kuwasilisha maombi ya kutaka kuongezwa mshahara kutoka Shilingi
Milioni 2 hadi 7 wakati wa utawala wa Malinzi.
Alipoulizwa na
wakili Rweyongeza kwamba Malinzi alikataa kumuongeza mshahara, Wambura alidai
kuwa si kweli, lakini alipeleka maombi hayo tena wakati wa utawala wa Rais wa
sasa wa TFF, Walles Karia ambapo ameidhinisha alipwe Shilingi Milioni 7 tangu
August 2017 hadi sasa.
Awali akiongozwa na
Wakili wa serikali, Shadrack Kimaro, Wambura alidai kuwa muhtasari wa June
5,2016 uliokuwa na ajenda ya kubadilisha watia saini wa akaunti za Benki za TFF
zilizopo Stanbic ni wa kughushi na kwamba yeye haufahamu.
Wambura amedai
anasema hayo kwa sababu alikuwepo katika kikao hicho cha June 5,2016 na
hakukuwepo na ajenda ya kubadilisha watia saini wa benki wa TFF kwa kumtoa
Edgar Masoud na kumuingiza Nsiande Mwanga.
Baada ya kueleza
hayo, kesi hiyo imeahirishwa hadi May 28 na 29 , 2018 kwa ajili ya kuendelea
kusikiliza kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka.
Katika kesi hiyo
washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine, Mhasibu wa TFF,
Nsiande Mwanga. Pia Meneja wa Ofisi wa (TFF),Miriam Zayumba na Karani wa TFF,
Flora Rauya.
Kwa pamoja
washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 30 ikiwemo kula njama, kughushi, kujipatia
fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa USD 173,335 na Sh
43,100,000.



