Breaking News

Dkt. Mengi Kuanzisha Taasisi Ya Teknolojia Na Uvumbuzi

Image result for dk reginald mengi
Mwenyekiti wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi.

Na Maneno Selanyika -Dar Es Salaam

MWENYEKITI wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi, amesema anakusudia kuanzisha taasisi mpya ya  teknolojia na uvumbuzi  itakayosaidia kuongeza ajira kwa vijana katika sekta mbalimbali..

Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa mazungumzo na Balozi wa China hapa nchini, Wang Ke, alipomtembelea ofisini kwake.

Katika mazungumzo hayo, Mengi, alisema ameamua kupanua wigo katika uwekezaji na taasisi anayotarajia kuanzisha itajihusisha na masuala mbalimbali ya kilimo na uwekezaji wa masoko.

 “Hapa Tanzania tunayo ardhi nzuri yenye rutuba, inayoweza kustawi mazao ya aina tofauti yanayoweza kuuzwa katika mataifa yaliyoendelea na yenye idadi kubwa ya watu kama China na mengineyo,” alisema Mengi. 

Aidha Dkt. Mengi aliongeza kuwa hapa nchini kuna mazao udongo wenye rutuba ambao unaweza kustawisha mazao mbalimbali kama mihogo, maparachichi na mengineyo.

Naye Balozi Wang, alisema taifa lao limejikwamua katika umasikini kwa kuwa wananchi wake walikuwa wakifanya kazi kwa bidii bila kukata
tamaa.

Alisema matumizi ya rasilimali zilizopo ndiyo njia pekee iliyowafanya Wachina leo hii waonekane wamekua kiuchumi duniani.

 “Labda niwatake tu vijana kila mmoja afanye kazi kwa ubunifu na kutumia rasilimali zilizopo karibu naye ili kuongeza pato lake, familia na taifa kwa ujumla," alisema.

Pia alisema China ipo mstari wa mbele kusaidia watu wenye ulemavu wa aina mbalimbali, lengo likiwa ni kukuza uhusiano mzuri baina ya
makundi maalumu na jamii iliyowazunguka.