Waziri Prof Kabudi Izi Ndo Sababu Masheikh Wa Uamsho Kuchelewa Kufikishwa Mahakamani

Waziri wa Katiba
na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema masheikh wa Uamsho kuchelewa
kufikishwa mahakamani kunatokana na upelelezi kutokamilika, kwamba Serikali
imeomba ushahidi kutoka nje ya nchi.
Akizungumza
jana wakati akijibu hoja za wabunge zilizoibuka wakati wa mjadala
wa bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi mwaka 2018/19, Kabudi amesema
suala hilo halihusu wizara hiyo, kwamba linamhusu Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
“DPP ana uwezo wa kufungua
mashtaka na kuyafuta na hakuna mtu wa kuingilia . Na kwa sababu hawezi kuingia
bungeni nimemwomba anipe majibu kuhusu suala la masheikh wa uamsho. DPP
alikuwa Singida nimemuomba aje aniletee taarifa hapa,”amlisema.
Alisema kuwa suala
hilo ni nyeti na adhabu yake ni kubwa, hivyo ndio maana upelelezi umechukua
muda mrefu ili kuhakikisha wanapata taarifa za kutosha kabla ya kuwafikisha
mahakamani.
Hata hivyo,
alisema Serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha suala hilo linafikia mwisho.
“Na hii bahati
mbaya sana watu wanaojadiliwa wana hadhi ya masheikh lakini hawakuingizwa
kwenye tuhuma za ugaidi kama masheikh, kwa sababu tuhuma lazima tuchunguze
kwani wakitiwa hatiani adhabu yake ni kubwa,”alisema.
Alisema uchunguzi
huo unafanyika nje ya nchi na ndani ya nchi na kwamba wameomba ushahidi kutoka
nje ya nchi kuhusiana na tuhuma hizo.



