Salum Mwalimu Afungua Kesi Kupinga Ushindi Wa Maulid Mtulia Wa Kinondoni

Mtulia aliibuka mshindi kwa kura
30,313 dhidi ya 12,353 alizopata Mwalimu. Uchaguzi huo ulifanyika kutokana na
Mtulia kujivua ubunge wa jimbo hilo akiwa CUF na kujiunga na CCM iliyompitisha
kugombea.
Mwalimu amefungua kesi dhidi ya
Mtulia; msimamizi wa uchaguzi ambaye ni mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni na
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).
Mbali ya kesi ya msingi namba 129 ya
mwaka 2018, Mwalimu amefungua maombi ya kusamehewa au kupunguziwa kiwango cha
fedha anachopaswa kukiwasilisha mahakamani kama dhamana kwa ajili ya
usikilizwaji wa kesi hiyo.
Katika kesi ya msingi, Mwalimu
anaiomba mahakama itengue matokeo na itamke kuwa uchaguzi ulikuwa batili,
pamoja na mambo mengine akidai uligubikwa na kasoro nyingi na mwenendo mbaya.
Anadai Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia
Ackson wakati wa kampeni alitoa kauli za ubaguzi.
Katika hati ya madai , Mwalimu anadai
msimamizi wa uchaguzi alishindwa kutoa fomu (kiapo cha siri) kwa mawakala wake
wa vituo vya kupigia kura siku saba kabla ya uchaguzi kinyume cha Kanuni za
Uchaguzi za mwaka 2015.
Anadai bila sababu za msingi, msimamizi
wa uchaguzi alikataa na alishindwa kuteua mawakala mbadala wa vituo vya kupigia
kura licha ya kuwasilisha kwake majina ya mawakala hao yaliyopendekezwa.
Pia, anadai aliweka masharti mengine
kwa mawakala wa vituo vya kupigia kura akiwataka kuwa na kadi za utambulisho na
barua za utambulisho kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi, aliloliweka siku ya
upigaji kura.
Anadai msimamizi alishindwa
kuhakikisha usalama wa masanduku ya kupigia kura, hivyo kusababisha moja katika
kituo cha kupigia kura namba 3 kwenye Mtaa wa Idrisa, Kata ya Magomeni
kuhamishwa na watu wasiojulikana wakati wa upigaji kura na kurejeshwa nusu saa
baadaye.
Mwalimu anadai timu ya kampeni ya Mtulia
iliyomhusisha Dk Tulia ilitoa maneno ya ubaguzi na yaliyompa haki isiyo sawa
mpinzani wake.
Anadai maneno yaliyotolewa na Dk
Tulia ni “Mkimchagua Mtulia nitampanga kukaa karibu na waziri mkuu.”
Mwalimu anadai mtiririko wa kasoro,
ukiukwaji wa sheria na utaratibu uliathiri matokeo ya uchaguzi na demokrasia.
Mwanasiasa huyo anaiomba mahakama
ibatilishe matokeo yaliyompa ushindi Mtulia akidai uchaguzi haukuwa huru na wa
haki, hivyo ni batili.
Katika kesi za uchaguzi kila
anayefungua kupinga matokeo anapaswa kuwasilisha mahakamani Sh5 milioni kama
dhamana ya usikilizwaji wa kesi kwa kila mdaiwa. Kwa kawaida kesi za uchaguzi
wadaiwa wa msingi huwa watatu; mbunge aliyeshinda, msimamizi wa uchaguzi
aliyemtangaza mshindi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kama ilivyo kwa Mwalimu,
anapaswa kuwasilisha mahakamani Sh15 milioni kama dhamana ya usikilizwaji wa
kesi.
Hata hivyo, Sheria ya Uchaguzi inatoa
nafasi kwa mtu ambaye anadhani hana uwezo wa kupata kiasi hicho cha fedha
kuwasilisha maombi akiomba kusamehewa zote au kupunguziwa kiwango. Kama
mahakama itajiridhisha kuwa hana uwezo basi inaweza kumsamehe au kumpunguzia
kiwango na kumpangia itakachoona inafaa.
Mwalimu amewasilisha maombi
mahakamani akiomba asamehewe kabisa au impunguzie akidai si mbunge, hivyo hana
uwezo wa kuweka kiasi hicho cha fedha.
Mashauri hayo (kesi ya msingi pamoja
na maombi), yaliyopangwa kusikilizwa na Jaji Ignas Kitusi yalitajwa mahakamani
jana. Jaji Kitusi ameelekeza Mtulia apewe nyaraka za mashauri hayo baada ya
kubaini hajapewa.
Mwalimu aliwakilishwa na wakili Alex
Masaba, huku msimamizi wa uchaguzi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
wakiwakilishwa na Wakili wa Serikali, Benson Hoseah. Mashauri hayo
yaliahirishwa hadi Mei 14 yatakapotajwa.



